Friday, January 23, 2015

Polisi: Kina Halima Mdee walikaidi amri, wakatukashifu


Polisi: Kina Halima Mdee walikaidi amri, wakatukashifu
Mbunge wa Kawe, Halima Mdee na wenzake wanane wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Shahidi wa kwanza Inspekta Jacob Swai katika kesi inayomkabili Mbunge wa Kawe, Halima Mdee na wenzake wanane wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), amedai kwamba washtakiwa waliwakashfu polisi na kukaidi amri ya kuwazuia wasiandamane.
 
Kadhalika, amedai kuwa pamoja na Jeshi la Polisi kutoa ilani kwa wanachama hao kwamba watawanyike na kuwazuia wasiandamane, walikaidi na kulikashfu jeshi hilo kwamba ni vibaraka wa serikali.
 
Swai alitoa madai hayo jana mbele ya Hakimu Mkazi Janeth Kaluyenda, wakati akitoa ushahidi dhidi ya kesi ya kutotii amri halali ya Jeshi la Polisi na kufanya mkusanyiko usio halali. 
 
Akiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi Mohamen Salum, alidai kuwa Oktoba 14, mwaka 2014, saa 12:00 asubuhi, katika kikao cha utendaji cha kazi chini ya bosi wake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, alipokea taarifa kwamba Baraza la Wanawake Chadema (Bavicha), watafanya maandamano isivyo halali kwenda Ikulu ya Tanzania.
 
Alidai kuwa saa 4:00 asuhubi alipokea taarifa kupitia simu ya upepo kwamba Bavicha wamekusanyika Mtaa wa Ufipa, Kinondoni jijini Dar es Salaam na kwamba wanataka kuandamana na bango kwenda Ikulu.
 
"Nilipofika eneo la tukio na kikosi kazi changu tuliwakuta wenzetu wakiongozwa na Mrakibu wa Polisi, Tire… afande Tire alikuwa akitoa ilani kwa wanachama hao zaidi ya 20 walikuwa wamekusanyika eneo la Makao Makuu Chadema," alidai na kuongeza:
 
"Afande alitoa ilani kwamba watu wote waliokusanyika mahali pale watawanyike 'ilani ilani … watu wote mliokusanyika mahali hapa mnaarifiwa na serikali ya Tanzania kutawanyika kwa amani la sivyo tutamia nguvu' ndivyo alivyotoa ilani bosi wangu."
 
Alifafanua kuwa baada ya amri hiyo washtakiwa pamoja na wanachama wengine walikaidi na kutoa kashfa kwamba wameitwa Ikulu na rais kwa hiyo polisi hawana uwezo wa kuwazuia kuandamani.
 
Alidai kwa kuwa maandamano hayo hayakuwa halali, makundi manne tofauti ya jeshi hilo yaliingiza kazini kuzuia waandamanaji hao na kundi lake lilifanikiwa kuwakamata  mshtakiwa wa pili, tatu na wa sita.