Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo.
Taasisi ya Utawala Bora na Maendeleo (Cegodeta) imemtaka Rais Jakaya Kikwete kuinusuru nchi kwa kumwajibisha Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, na wale wote waliohusika na kashfa ya uchotwaji wa zaidi ya Sh. bilioni 300 kutoka akaunti ya Tegeta Escow kwa kupelekwa mahakamani na kuzirudisha fedha hizo ili kuondokana na kifungo cha kunyimwa misaada na wafadhili.
Aidha, Cegodeta imesema kiporo ambacho Rais Kikwete alimuweka Prof. Muhongo kimechukua muda mrefu, hivyo wananchi wanatarajia kuona waziri huyo akifukuzwa kazi.
Kauli hiyo ilitolewa jana jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa Cegodeta, Thomas Ngawaiya, na kufafanua kuwa sheria inasema kuwa kwa yeyote aliyetoa rushwa na aliyepokea wote wana kesi ya kujibu kwani ni kinyume cha sheria.
Ngawaiya alisema wote waliotajwa kuhusika na uchotwaji wa fedha hizo wanapaswa kushitakiwa na kuzirudisha kwani wafadhili wanataka kuliona hilo na sio kujiuzulu pekee.
"Prof. Muhongo anapaswa kujiuzulu kwani taratibu za uongozi bora anazijua, hivyo sioni sababu ya yeye kung'ang'ania wizarani kwani uchafu wote huu umetokea katika ofisi yake," alisema Ngawaiya.
Ngawaiya alisema Serikali inapaswa kufahamu kuwa wananchi hawataelewa kuona wale wote waliotanjwa hawajiuzulu bila kufikishwa mahakamani.
"Hivi sasa kuna miradi mbalimbali inaweza kuwa imekwama kutokana na kusitishwa misaada na wafadhili, mishahara itakwama na hata maendeleo yatasimama hivyo kutengeneza bomu katika suala la ajira," alisema.
Ngawaiya ambaye aliwahi kuwa Mbuge wa Moshi Vijijini na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kilimanjaro, alisema hivi sasa wananchi wamejenga chuki dhidi ya CCM kutokana na kashfa hii ya ya Escrow, hivyo Serikali inabidi kuirudisha imani kwa kuwawajibisha waliohusika.