Friday, January 23, 2015

Mwambalaswa ang'ang'ania uenyekiti Kamati Bunge



Mwambalaswa ang'ang'ania uenyekiti Kamati Bunge
Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Victor Mwambalaswa.

Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Victor Mwambalaswa, anaonekana kung'ang'ania nafasi hiyo huku Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala, William Ngeleja, akisema anaheshimu kauli ya Spika wa Bunge, Anna Makinda, kwamba wenyeviti wa kamati za bunge ambao walihusika katika kashfa ya Tegeta Escrow, wameshajiuzulu.
 
Juzi Makinda alisema kwamba anachojua wenyeviti hao wameshajiuzulu kufuatia azimio namba nane la Bunge lililotolewa mwishoni mwa mwaka uliopita  la kuwataka kufanya hivyo.
 
Jana tulishindwa kumpata Mwambalaswa wakati wa mapumziko ya kikao cha Kamati baada ya kuelezwa kwua alikuwa anajiandaa kuendelea na kikao.
 
 Hata hivyo, mmoja wa maofisa wa Bunge alisema kuwa, Mwambalaswa aliongoza kikao cha asubuhi kwa kuwa makamu wake hakuwapo na kwamba baada ya kufika Makamu Mwenyekiti angeendelea kuongoza kikao hicho kama alivyokuwa akifanya hapo awali hata kabla ya kutolewa kwa kauli hiyo ya Spika.
 
"Mwambalaswa yupo…kwa sasa hivi huwezi kumuona kwa sababu anaongoza kikao," alisema mmoja wa wabunge wa kamati hiyo na kuongeza:
 
"Asubuhi Mwambalaswa aliongoza kikao kwa sababu makamu mwenyekiti alikuwa hayupo...lakini sasa ameshafika ataendelea kuongoza kikao," alisema ofisa huyo.
 
Kwa mujibu wa ofisa huyo, Mwambalaswa alishajiuzulu muda mrefu hata kabla ya kutolewa kwa kauli ya Spika Makinda na kwamba aliyekuwa anaongoza vikao vya kamati hiyo ni makamu mwenyekiti wake ambaye ndiye mwenye taarifa zote za vikao.
Hata hivyo alisema hadi wakati huo walikuwa hawajapokea taarifa kamili ya maandishi kutoka kwa Spika na kuwa huo ndiyo utaratibu.
 
Pamoja na Mwambalaswa, wenyeviti wengine waliotakiwa kujiuzulu ni Mwenyekiti wa Kamati ya za Bajeti, Andrew Chenge na Katiba, Sheria na Utawala, Ngeleja.
 
Hata hivyo, Ngeleja alipoulizwa jana, alijibu kwa kifupi kuwa kauli ya  iliyotolewa na Spika Makinda ni sahihi bila kutaka kufafanua kama atajiuzulu ama la.
 
Alitoa kauli hiyo baada ya kumalizika kwa kikao cha kamati hiyo katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam.
 
Hata hivyo mmoja wa wajumbe  wa kamati hiyo, akizungumza na waandishi wa habari, alisema, kikao cha jana cha kamati hiyo kiliongozwa na mjumbe, Nyambari Nyangwine kutokana na Ngeleja na Makamu wake, Gosbert Blandes kutokuwapo.
 
Hivi karibuni, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti, Dk. Festus Limbu, alisema, mwenyekiti wake Chenge, hajajiuzulu hajajiuzulu ingawa kamati ilikuwa imemweka pembeni asiongoze vikao kwani alikuwa anasubiri taarifa kutoka kwa Spika.