Sunday, January 25, 2015

Breaking news: MGOMO WA WAENDESHA DALADALA JIJINI MWANZA LEO



Breaking news: MGOMO WA WAENDESHA DALADALA JIJINI MWANZA LEO

WAENDESHA magari ya kusafirisha abiria katika ya Jiji la Mwanza maarufu kama daladala leo wamefanya mgomo na kuziba njia zote zinazoingia mjini kutokana na maeneo waliyokuwa wanaegesha magari yao kwa ajili ya kusubiri abiria (stendi) kugawiwa wafanyabiashara ndogondogo maarufu kwa jina la machinga kwa ajili ya shughuli zao.

Hali hiyo imetokea leo asubuhi katika eneo la Stendi ya Tanganyika na Stend ya Soko Kuu jijini Mwanza ambapo yanaegesha magari ya kwenda Airport, Ilemela, Bwiru na Mwaloni ambapo madereva hao waliziba njia zote zinazo ingia kwenye maeneo hayo.



Mwenyekiti wa waendesha daladala Mkoani Mwanza, Hassan Dede Petro alisema hali hiyo imejitokeza kutokana na wafanyabiashara hao kuanza kugawana maeneo kwenye stendi hizo bila uongozi wa waendesha daladala kuwa na taarifa yeyote kuhusu suala hilo.

Daladala zikiwa zimeegeshwa wakati wa mgomo.

''Hali hii imejitokeza kwa sababu ya wafanyabiashara wadogodogo kuanza kujigawia maeneo katika eneo letu ambalo tunaegesha kwa ajili ya kusubiri wateja wetu (abiria)'' Alisema Petro.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa wafanyabiashara ndogondogo 'machinga' Said Tembo alisema walichukua uamuzi huo kutokana na kupata ruhusa kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Magesa Mulongo kuwa watumie maeneo hayo kwa shuhuli zao za kufanyabiashara kwenye maeneo ya stendi hizo.