Kivuko cha Mv. Magogoni
Wakazi wa Feri, Dar es Salaam, wameiomba Serikali kukifanyia marekebisho kivuko cha MV Magogoni kinachofanya safari zake kati ya Kivukoni na Kigamboni ambacho kimekuwa kilaharibika kila mara na kusababisha usumbufu kwa abiria.
Hatua hiyo imefuatia matukio ya kuharibika mara kwa mara nyakati za usiku na kuchukua muda majini huku kikiwa na abiria na magari.
Fadhili Mbaga, mkazi wa Kigamboni, alisema, Serikali inapaswa kuangalia kwa makini suala la usalama wa abiria wa Feri ambao wanatumia usafiri huo, kutokana na kivuko hicho kutokuwa na sifa za kusafirisha abiria wengi na mizigo kwa wakati.
"Abiria tumekuwa na wasiwasi na huu usafiri kwani mara nyingi injini ya kivuko hiki siyo nzima na kusababisha ofu kubwa kwetu," alisema.
Anna Mwasombe, mwanafunzi wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, alisema kutokana na ubovu wa kivuko hicho, abiria wengi wasiokuwa na haraka hulazimika kusubiri kupanda kivuko cha MV Kigamboni.
"Mara nyingi kivuko hiki kikiwa kinafanya safari zake hutumia saa nyingi kufika upande wa pili kutoka na kuelemewa, hivyo kusababisha abiria kutumia muda mrefu kufika kutokana na kutembea taratibu," alisema.
Samson Gama, alisema Serikali kwa kushirikiana na Wakala wa Ufindi na Umeme (Temesa) inapaswa kufanya ugaguzi kila wakati ili kuhakikisha vivuko vyote vinakuwa katika hali nzuri na salama kusafirisha abiria.
Hata hivyo, Paparazi ilimtafuta Afisa Habari Temesa kutolea ufafanuzi kuhusiana na malalamiko hayo, lakini simu yake haikupatikana.