WATU wawili wakazi wa wilaya ya Mlele mkoani Katavi wameuawa kikatili ambapo mmoja amecharangwa kwa mapanga na mwili wake kukatwa vipande vipande kisha kuzikwa shambani kwake na mwingine kuchinjwa na watu wanaodaiwa kuwa wa familia yake.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Katavi, Dhahiri Kidavashari alithibitisha kutokea kwa mauaji hayo na kusema aliyekatwa vipande ni Minza Mwanalushinga (26) mkazi wa kitongoji cha Vilolo, katika kijiji cha Manga, kata ya Kibaoni wilayani Mlele.
Mwingine kwa mujibu wa Kamanda Kidavashari ametambuliwa kuwa ni Giti Mawiti (53) mkazi wa kijiji cha Tupindo - Minyoso wilayani Mlele ambaye inadaiwa alikutwa amechinjwa.
Akisimulia tukio hilo Kamanda Kidavashari alisema tukio la kwanza lilitokea Januari 15, mwaka huu, saa moja jioni katika kitongoji cha Vilolo ambapo Mwanalushinga anadaiwa aliondoka alfajiri kwenda kuchota maji umbali wa kilomita moja na wakati akirejea nyumbani kwake alivamiwa na watu wasiojulikana na kumburuza hadi shambani kwake kisha wakamcharanga kwa mapanga na kumkata vipande vipande na kuvifukia shambani kwake.
Kwa mujibu wa Kamanda huyo, tayari Jeshi la Polisi mkoani humo linawashikilia watu wawili akiwemo mume wa marehemu, Kimbulu Joseph na jirani yake Joseph Abel kwa uchunguzi zaidi.
Katika mkasa mwingine ambao unadaiwa kutokea Januari 16, mwaka huu, saa tatu usiku katika kitongoji cha Tupido, marehemu Giti Mawiti (53) alikuwa nyumbani kwake akisumbuliwa na tumbo ndipo alipowaamsha watoto wake Kanedeku Giti (26), Kabula Giti (21) na Nyanzobe Giti (16) ili wamchemshie maji anywee dawa huku yeye akiwa amejilaza barazani.
Kwa mujibu wa Kamanda Kidavashari ghafla alitokea mtu akiwa na tochi yenye mwanga mkali na kuwamulika machoni ambapo watoto wote hao walikimbia na kumwacha baba yao ambapo muda mfupi baadaye wakiwa mafichoni walimsikia baba yao akipiga kelele za kuomba msaada.
Inadaiwa kutokana na hofu waliyokuwa nayo watoto hao walisita kurejea nyumbani kumsaidia baba yao mzazi.
Kamanda Kidavashari amethibitisha kuwa Jeshi la Polisi mkoani humo linamshikilia mtoto wa marehemu Kanedeku Giti (26) akihusishwa na kifo hicho cha baba yake mzazi.
Kamanda Kidavashari amethibitisha kuwa Jeshi la Polisi mkoani humo linamshikilia mtoto wa marehemu Kanedeku Giti (26) akihusishwa na kifo hicho cha baba yake mzazi.