Friday, July 04, 2014

Balozi Seif Ali Iddi autaka Uongozi wa Mamlaka ya uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Zanzibar { ZIA } kuwa wabunifu



Balozi Seif Ali Iddi autaka Uongozi wa Mamlaka ya uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Zanzibar { ZIA } kuwa wabunifu
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameuagiza Uongozi pamoja na Watendaji wa Mamlaka ya uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Zanzibar { ZIA } kuwa wabunifu katika kuandaa utaratibu mzuri unaokwenda na wakati ambao utaondoa usumbufu kwa wasafiri wanaotumia uwanja huo.

Alisema watendaji hao pia wanapaswa kubadilika na kwenda na wakati kulingana na huduma wanazotoa kwa wasafiri hasa wakizingatia kwamba uwanja huo hivi sasa unaendelea kuimarishwa katika hadhi na kiwango cha Kinachokubalika kimataifa.

Balozi Seif Ali Iddi alitoa agizo hilo wakati alipofanya ziara fupi ya ghafla kwenye uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Zanzibar kufuatia malalamiko mbali mbali aliyokuwa akiyasikia kutoka kwa baadhi ya abiria kutokana na huduma zinazotolewa uwanjani hapo .

Balozi Seif alisema utaratibu uliopo hivi sasa ni vyema ukaimarishwa zaidi ili kupunguza bughdha pamoja na kuwapa faraja abiria ambao wengi kati yao huwa tayari wameshachoka kutokana na uchovu wa safari zao za Kimataifa.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar uliutaka uongozi huo wa Mamlaka ya Uwanja wa Ndege wa Zanzibar kukaa pamoja na Idara ya Uhamiaji pamoja na taasisi nyengine zinazokusanya mapato kiwanjani hapo katika kulitafutia ufumbuzi wa haraka tatizo la urasimu unaosababisha msongamano mkubwa wa wasafiri.

Mapema Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uwanja wa Ndege wa Zanzibar Nd. Said Iddi Ndombogani alisema mamlaka hiyo inaendelea na juhudi za kukamilisha matengenezo ya banda la wasafiri ili kuondosha malalamiko ya abiria kuteremka mbali na eneo la kupata huduma zingine.

Alifahamisha kwamba Mamlaka inaendelea kuzingatia vigezo vya Kimataifa katika kutoa huduma kwa wasafiri wanaotumia usafiri wa anga ambao humtaka abiria anayesafiri ateremke kwenye gari masafa ya mita mia Moja na eneo analotakiwa kupata huduma kwa ajili ya safari yake.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiuagiza Uongozi wa Mamlaka ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Zanzibar { ZIA } kuwa wabunifu katika kutoa huduma zinazokwenda kimataifa baada ya kufanya ziara ya ghafla katika uwanja huo. Kushoto ya Balozi Seif ni Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uwnja wa Ndege wa Zanzibar Nd. Said Iddi Ndombogani na Katibu Mkuu Wizara ya Maiundombinu na Mawasiliano Zanzibar Dr. Juma Malik Akili.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Zanzibar Nd. Said Iddi ndombogani kulia akimpatia maelezo Balozi Seif aliyepo kati kati wakati alipofanya nziara ya ghafla kiwanjani hapo. Kulia yao ni Katibu Mkuu Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano Zanzibar Dr. Juma Malik Akili.
Katibu Mkuu Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano Zanzibar Dr. Juma Malik Akili akimfafanulia jambo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alipofanya ziara fupi kwenye uwanja wa ndege wa Zanzibar.
Baadhi ya abiria wa Kimataifa walioingia Zanzibar kwa usafiri wa anga wakipata huduma zitakazowapa fursa za kuwepo nchini kwa taratibu zilizowekwa kisheria.
Balozi Seif akiagizwa kuandaliwa utaratibu wa utoaji huduma wa ubia kwa watendahji wa uwanja wa ndege wa Zanzibar ili kupunguza msongamano wa abiria kiwanjani hapo. Picha na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ.