Sunday, April 19, 2015

LUKUVI AWAPA MWEZI MMOJA MAOFISA WA ARDHI DAR



LUKUVI AWAPA MWEZI MMOJA MAOFISA WA ARDHI DAR


Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi (pichani), ametoa mwezi mmoja kwa maafisa ardhi wa manispaa za jiji la Dar es Salaam, kusikiliza na kupata ufumbuzi wa kero za ardhi za wananchi vinginevyo hatua zitachukuliwa kwa watendaji waliohusika kusababisha kero hizo.


Kadhalika, alisema maafisa ardhi wengi wanashiriki kudhulumu, kunyanyasa, kupora haki za waonyonge na kuwapa matajiri huku wakishiriki utakatishaji fedha.
Akizungumza  na wafanyakazi wa Wizara na Manispaa za Jiji hilo, alisema wizara hiyo inaongoza kwa kero kwa wananchi na kwamba ndiyo sekta pekee ambayo inaidhalilisha na kuichafua serikali kutokana na kuwa na walafi ambao wanashirikiana na matapeli.
Alisema anataka kuona kero za kuporwa viwanja, uuzaji holela wa viwanja kuuza kwa mtu zaidi ya mmoja,  kuwanyima hati zao wananchi, zinamalizwa kwa haraka kabla hajaingia kuchukua hatua mwenyewe.
Alisema wapo watumishi ambao wamejimilikisha viwanja zaidi ha 20 hadi 30 na wanafuta hati za watu na kuwapa watu wengine mamlaka ambayo siyo yao bali ya Rais.
Alisema amefanya utafiti wa miezi miwili na kubaini madudu ya kutisha na jiji la Dar es Salaam linaongoza kwa upimaji, umilikishwaji mbovu na kutoa kiwanja kimoja kwa zaidi ya watu wanne, uvunjifu wa kanuni za ardhi na kutembea na mafaili mtaani kwa ajili ya kupanga utapeli na matapeli.
"Manispaa ya Kinondoni inaongoza kwa uvunjifu wa kanuni na sheria kwa asilimia 85, watu wameonewa sana , maafisa ardhi wanatumia mamlaka yao vibaya, watu wameporwa haki zao, hati, ofa, mnashirikiana na matapeli wanaojulika wanapora ardhi za wanyonge na kuwapata matajiri," alisema.
Alisema jiji hilo halina usimamizi wa kanuni na sheria ya ardhi, wanatumia ovyo madaraka yao, na kwamba wengi hawakai ofisini bali wanazunguka mitaani na mafaili ya watu kwa ajili ya kutafuta fedha na ofisi ni kama kichochoro na huduma inatolewa mwa kumwangalia mtu usoni.
Waziri Lukuvi alisema hakuna utunzaji mzuri wa kumbukumbu na unafanywa kwa makusudi kupoteza ushahidi kwa kutoa nyaraka za mtu mwenye hati wa zamani na kuweka za mtu mwingine.
Alisema pia maafisa hao wanaloweka kwenye maji na majani ya chai nyaraka za watu ili zionekane za zamani na wino ikiwa ni mpya.
Alionyesha nyaraka mbalimbali ikiwamo iliyowekewa maji ya majani ya chai ili ionekane ni karatasi kukuu huku wino ukiwa mpya.
Alimtaja Afisa Ardhi wa Manispaa ya Ilala, Batoni Ruta, ambaye alimwandikia barua Waziri akimtaka kumueleza juu ya maeneo mawili ambayo yalifutwa na rais akitaka kuwapa watu wengine.
Mtumishi mwingine ni Afisa Ardhi wa Manispaa ya Kinondoni ambaye kabla alikuwa wilayani Arumeru, Nicodemas Hiro, ambaye alitoa ofa kwa mwekezaji wa kampuni ya Tanzania tip Plantation aliyekuwa mmiliki wa shamba lenye ukubwa wa ekari 1359 ambaye alinyang'anywa na kupewa Chuo Kikuu cha Nelson Mandela.
Alisema licha ya mtumishi huyo kujua kuwa rais amefuta hati hiyo, lakini alimpa tena mwekezaji huyo na sasa ameiburuza serikali mahakamani anaidai Sh milioni 13.
Alisema serikali imesitisha zoezi la utoaji wa hati hadi uchunguzi utakapofanyika kuonyesha upimaji, utoaji kiwanja kuwa ulizingatia sheria na kanuni.
Lukuvi alisema ardhi ndiyo stahiki ya kila mnyonge lakini inauzwa ghali kwa lengo mahususi ili watumishi waweze kumiliki mapande makubwa ya ardhi, huku maeneo mengine wakiyaonyesha kwenye ramani kama ni maeneo ya mabonde kumbe wameyatenga mahususi kwa ajili yao ili baadaye wauze kwa bei ya ulanguzi.
CHANZO: NIPASHE