Thursday, October 30, 2014

TANESCO KUMALIZA KERO YA UMEME DAR KESHO NOVEMBA MOSI



TANESCO KUMALIZA KERO YA UMEME DAR KESHO NOVEMBA MOSI
Na  Mwene Said 



Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), limesema usumbufu wa kukatika kwa umeme uliojitokeza wiki moja iliyopita limetokana na usafi wa visima vya mafuta na kwamba hadi kufikia kesho hali itarudi kawa kawaida.

Akizungumza na waandishi wa habari katika ukaguzi wa mtambo wa kuchuja umeme Tandika,  jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco, Bw.Felchesmi Mramba (pichani)  alisema usumbufu huo ulitokana na Kampuni ya Pan Afrika kufanya usafi kwenye visima vyake vya mafuta.
"Kutokana kufanyika usafi wa visima vya mafuta gesi ni ndogo na kwamba imeathiri maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam... hali hiyo itakwisha leo na kuanzia kesho Novemba Mosi hali ya umeme itakuwa ya kawaida na usumbufu kwa wateja wetu utaisha" alisema Mramba.
Mbali na usumbufu huo, Mramba alisema shirika lake lina mkakati mkubwa wa kuondoa kero ya umeme kwa wakazi wa Mbagala, Kurasini, Mkuranga, Kigamboni, Chamazi, Tuangoma, Kurasini na Mtoni Kijichi wanaopata hudumu kutoka kituo cha Ilala sasa watahamishiwa kituo cha Kipawa kupitia Tandika.
Akifafanua zaidi alisema kituo cha Kipawa kitapeleka umeme kituo cha Tandika ambacho kitachuja na kupatikana Mega Wati 12.5 zitakaboresha huduma kwa wakazi wa maeneo hayo.
"Hadi kufikia Aprili mwaka 2015 shirika litatoa huduma nzuri kwa wakazi wa Dar es Salaam na kero ya umeme itakuwa historia... "alisema Mkurugenzi huyo wakati akikagua ukarabati wa kituo cha kuchuja umeme kilichopo Tandika, Wilaya Temeke.