Sunday, August 09, 2015

UCHAGUZI MPYA UWT VIGOGO CHALI, SURA MPYA ZATAWALA



UCHAGUZI MPYA UWT VIGOGO CHALI, SURA MPYA ZATAWALA

Wabunge wa muda mrefu wa viti maluum wa Chama cha Mapinduzi (CCM), wamebwagwa katika uchaguzi wa wawakilishi na wabunge kupitia makundi mbali mbali ya Umoja wa Wanawake (UWT).



Makundi hayo ni pamoja ya Watu wenye ulemavu, Vijana, Wafanyakazi, Taasisi zisizo za Kiserikali, Vyuo vikuu na Wazazi, ambayo yameibuka na sura mpya.

Vigogo waliangushwa katika kundi la watu wenye ulemavu ni Al-Shamaa Kwegyir, Magreth Mkanga na Riziki Lulida.

Kundi la Taasisi zisizo za kiserikali (NGO's) aliyeshindwa ni Dk. Maua Daftari na katika kundi wafanyakazi ni Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki, Shyrose Banji.

Kwa upande wa wasanii, walioanguka ni Irene Uwoya na Khadija Taya maarufu kama Keisha.

Baadhi ya watoto wa vigogo waliangushwa katika uchaguzi huo ni Jacqueline Mzindakaya na Sinzo Hamis Mgeja.

Akitangaza matokeo hayo, msimamizi wa uchaguzi huo, Zakhia Meghji, aliwataja walioshinda katika kundi la wawakilishi la watu wenye ulemavu na kura zao kwenye mabano kuwa ni Stela Alex (51) na Mtangazaji wa TBC, Amina Mollel (44).

Aidha walioshinda kundi la wafanyakazi ni aliyekuwa Naibu waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angellah Kairuki (143) na Hawa Chakoma (47). Walioshinda kundi la NGO's ni Dk. Getrude Rwakatale (82) na Rita Mlaki (59).

Kupitia kundi la vyuo vikuu, washindi ni Dk. Jasmine Tiisekwa (61), ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini na Esther Mmasi (46).

Kundi la vijana kutoka Bara na Zanzibar ni Khadija Nasri Ally (117), Munira Mustafa Khatibu (105), Nadra Juma Mohammed (103) na Time Bakari Sharifu (91).

Wengine ni Halima Bulembo (109), Zainab Katimba (77), Julia Masaburi (62), Mariam Ditopile Mzuzuri (62), Mariam Kangoye (57) na Sophia Kizigo (42).

Aliwataja walioshinda katika Kundi la Wazazi kuwa ni Catherine Peter Nao (74) kutoka Zanzibar na matokeo kwa upande wa Tanzania bara yakiwa yanaendelea kutolewa.

Kuhusu kundi la wabunge Viti maalum kutoka kila mkoa, Katibu wa Idara ya Oganizesheni UWT, Riziki Kingwande, alisema wanawake walioshinda katika nafasi ya kwanza na ya pili kwenye kila mkoa wataingia moja kwa moja bungeni  kulingana matokeo ya urais.