Sunday, August 09, 2015

KARIBU NUSU YA TANZANIA INA MIAMBA YA GESI NA MAFUTA



KARIBU NUSU YA TANZANIA INA MIAMBA YA GESI NA MAFUTA

KARIBU nusu ya eneo la Tanzania, imetajwa kuwa na miamba inayohifadhi rasilimali muhimu ya kiuchumi ya mafuta na gesi, ambalo bado halijafanyiwa utafiti.


Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Dk James Mataragio, aliyasema hayo hivi karibuni katika Jiji la San Antonio nchini Marekani, iliposhiriki katika moja ya mikutano mikubwa duniani, inayojumuisha washiriki na wadau wa kimataifa wa mafuta na gesi. Mkutano huo pia uliambatana na maonesho ya kimataifa.
Kutokana na fursa hiyo, amesema TPDC iko mbioni kufanya utafiti wa kitaalamu uitwao "Airborne Gravity Gradiometer Survey" katika maeneo ya nchi kavu Kusini-Mashariki mwa Pwani ya Tanzania na upande wa Mashariki mwa Bonde la Ufa.
Utafiti huo kwa mujibu wa Dk Mataragio, unatarajiwa kuanza mwezi huu na utasaidia kuongeza thamani ya maeneo hayo kwa kutambua maeneo yenye uwezekano mkubwa wa kuhifadhi rasilimali za mafuta na gesi na utajumuisha eneo lenye ukubwa wa kilometa za mraba 30,000.
Mbali na utafiti, pia amesema TPDC, inaendelea kutekeleza dhima yake ya kukuza uwekezaji katika sekta hiyo ya mafuta na gesi.
"Katika kipindi hiki ambapo bado hali ya sekta ya mafuta na gesi iko chini kutokana na kushuka kwa bei ya mafuta, ni muhimu sana kwa nchi kama zetu ambazo bado zina fursa nyingi za utafiti wa mafuta na gesi, kujitangaza zaidi ili kuvutia wawekezaji wakubwa," alisema.
Mkurugenzi wa shughuli za mkondo wa chini, Dk Wellington Hudson alisema; "Mkutano huu umelenga kuangalia teknolojia mpya ya kutafuta mafuta na gesi ambayo ni tofauti na teknolojia ile ya kawaida. "Wenzetu wa Marekani ndio nchi pekee iliyoweza kuzalisha rasilimali hizi zijulikanazo kama unconventional resources," alisema.
Teknolojia hiyo ni inayoruhusu kutafuta mafuta na gesi katika miamba ambayo kwa njia ya kawaida ya utafiti isingewezekana kuzalisha.
HABARI LEO