Wednesday, August 27, 2014

RAIS KIKWETE KUZINDUA PROGRAMU YA UIMARISHAJI WA MIPAKA YA KIMATAIFA MKOANI KAGERA


RAIS KIKWETE KUZINDUA PROGRAMU YA UIMARISHAJI WA MIPAKA YA KIMATAIFA MKOANI KAGERA
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Kikwete anatarajia kuwa mgeni rasmi katika  uzinduzi wa programu ya  uimarishaji wa mipaka ya kimataifa kwa lengo la kuhuisha alama zilizopo na kuweka mpya katika maeneo ya  mipaka ya Tanzania ambayo awali yalikuwa yametengwa na mito na baadaye mito hiyo kukauka .

  Programu hiyo inayofanywa na wataalam wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi itazinduliwa rasmi Agosti 28, katika eneo la mpaka kati ya Tanzania na Burundi la Mugikomero wilayani Ngara mkoani Kagera kwa upande wa Tanzania na eneo la Nteritare  kwa upande wa Burundi.

  Aidha, itahusisha ujenzi na uwekaji wa vigingi vya mipaka, Marais wa nchi za Burundi na Tanzania kutembelea baadhi ya maeneo yenye alama za mipaka na kisha kuzungumza na wananchi waishio mpakani. Katika tukio hilo Rais Jakaya Kikwete anatarajia kumpokea mwenzake wa Burundi, Rais Pierre Nkurunziza atakayewasili nchini Tanzania kushuhudia zoezi hilo akitokea nchini Burundi kupitia mpaka wa Kabanga ulioko wilayani Ngara.

  Kaimu Katibu Tawala wa wilaya ya Ngara Bw. Hussein Seif akizungumzia maandalizi ya shughuli hiyo amesema kuwa wilaya hiyo imejipanga kuhakikisha kuwa programu hiyo inatekelezwa kwa ufanisi katika maeneo yote ya wilaya ya Ngara yanayopakana na nchi ya Burundi.

Naye Mkurugenzi Msaidizi wa Topographia na Giodosia wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. James Mtamakaya akizungumzia zoezi hilo amesema kuwa tayari maeneo mbalimbali ya mipaka ya Tanzania yameshapitiwa na zoezi hilo likiwemo eneo la mpaka kati ya Tanzania na Uganda.

 Ameyataja maeneo mengine kuwa ni eneo la Tanzania na Rwanda ambalo bado linatenganishwa na mto Kagera, eneo la mpaka kati ya Tanzania na Msumbiji, Tanzania na Kenya pamoja na zoezi la uimarishaji wa mpaka kati ya Burundi na Tanzania ambalo linaendelea kufanyika.
Kaimu Katibu Tawala wa wilaya ya Ngara Bw. Hussein Seif akitoa ufafanuzi kwa wajumbe wa maandalizi ya shughuli ya uzinduzi wa Programu ya uimarishaji wa mipaka ya Kimataifa wa wilaya ya Ngara itakayozinduliwa na Rais Jakaya Kikwete eneo la Mugikomero mpakani mwa Tanzania na Burundi. Wanaoonekana nyuma ni raia wa Burundi waishio mpakani.
Raia wa Burundi wakiwa nyuma ya alama ya mpaka inayotenganisha Tanzania na Burundi. Serikali kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi inaendelea na zoezi la kuhuisha mipaka hiyo ya kimataifa.
Moja ya Shamba la ndizi lililopandwa katikati ya eneo la mpaka kati ya Tanzania na Burundi ambalo kwa sheria za kimataifa haliruhusiwi kufanyiwa shughuli yoyote.
Bw. Israel Paul akipaka rangi moja ya alama ya mpaka unaotenganisha Tanzania na Burundi eneo la Mugikomero, wilayani Ngara kufuatia Programu inayoendelea ya uhuishaji wa mipaka ya kimataifa.

Viongozi wa wilaya ya Halimashauri ya Wilaya ya Ngara wakikagua moja ya eneo la mpaka wa Kabanga unaotenganisha Tanzania na Burundi ambapo Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania atampokea Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza.
Moja ya alama ya mpaka unaotenganisha Tanzania na Burundi ikiwa imekamilika katika eneo la Mugikomero, wilayani Ngara kufuatia Programu inayoendelea ya uhuishaji wa mipaka ya kimataifa.