Monday, August 03, 2015

NSSF, APOLLO WANAVYOJIPANGA KULETA MATIBABU YA INDIA NCHINI



NSSF, APOLLO WANAVYOJIPANGA KULETA MATIBABU YA INDIA NCHINI
Rais Kkwete aiongea              na timu ya viongozi wa
Kwenye sekta ya afya, inaaminika kuwa India ni mkombozi wa uhai wa Watanzania wengi kwa kuwa matibabu yaliyoshindikana hapa nchini yameweza kufanyika kwa ufanisi nchini humo.

Mpango huu umekuwa ukifanyika kutokana na hospitali kubwa nchini kukosa vifaa vya kisasa na wakati mwingine upungufu wa wataalamu bingwa katika fani kadhaa nyeti.
Miongoni mwa matatizo ambayo yamekuwa yakiwalazimisha wagonjwa wengi hapa nchini kupelekwa India ni upasuaji wa ubongo, moyo, figo na ini. Vilevile kuna wagonjwa wanaoenda kwa lengo la kubadili au viungo vilivyoathirika.

Mipango ya wagonjwa kupelekwa India imekuwa ikifanywa kwa namna mbili; ipo inayoratibiwa kwa msaada wa Serikali, hasa wale wagonjwa wasio na uwezo na pia wapo wanaoenda kwa gharama zao binafsi au kampuni za bima.
Katika kuratibu matibabu, moja ya hospitali ambayo imekuwa ikitumika sana nchini India ni Hospitali za Apollo, ambazo kwa sasa jina lake limezoeleka kwa wengi.
Juni 17 hadi 21, mwaka huu, Rais Jakaya Kikwete alitembelea India na kuwa na mazungumzo na Serikali ya India na baadaye alizuru Hospitali ya Apollo ambako alionana na timu ya madaktari na wauguzi.
Akiwa na Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi, Rais Kikwete aliishukuru India kwa misaada endelevu kwa Tanzania na kusema kuwa nchi hizo zimeamua kuendeleza uhusiano zaidi.
Rais Kikwete, akiwa na timu ya watendaji wa Serikali, alijadiliana mambo mengi na wataalamu bingwa katika Hospitali za Apollo na aliwahamasisha kuharakisha mpango wa kusogeza huduma za afya nchini Tanzania ili kupunguza gharama za Watanzania kwenda India.
Alihamasisha utekelezaji wa makubaliano kati ya Serikali ya Tanzania kupitia Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) na Hospitali ya Apollo.
Msimamizi Mwandamizi wa Majengo wa NSSF, Injinia John Ndazi anaeleza makubaliano ya NSSF na Apollo yanahusu: "Ujenzi wa hospitali ya kisasa na uanzishwaji wa kliniki ya kisasa nchini Tanzania na zote zitaendeshwa na madaktari bingwa pamoja na wataalamu wengine kutoka Hospitali za Apollo nchini India."
Anasema kwa kuanzia, wataanza na kliniki ambao itakuwa kwenye jengo lao lililopo katika makutano ya Barabara za Bibi Titi na Mrogoro jijini Dar es Salaam.
Mipango ya kliniki hiyo, anaielezea ipo kwenye hatua za mwisho na wakati wowote mwaka huu, itakuwa tayari kwa ajili ya wataalamu hao kutoka India kuanza kuonana na wagonjwa. Hata hivyo, taratibu na mfumo wa wagonjwa kuwaona wataalamu hao, anasema utatangazwa baadaye na uongozi wa NSSF.
Anasema uanzishwaji wa kliniki hii utafuatiwa na ujenzi wa hospitali ya kisasa hapo baadaye ambayo itaendeshwa na wataalamu kutoka Hospitali ya Apollo.
Anasema hospitali hiyo kubwa itajengwa eneo la Kigamboni, jijini Dar es Salaam na kwamba tayari michoro imekamilika na kilichobakia na mipango ya kumpata mjenzi aanze kazi hiyo.
"Uanzishwaji wa kliniki hii uko katika hatua za mwisho na uzinduzi wake unatarajiwa kufanyika mnamo mwezi Septemba, 2015," anasema Injinia Ndazi.
Anauelezea ujio huo wa wataalamu hao bingwa kuwa watafanya kazi nchini na wakati huohuo wataalamu wazalendo  watapata uzoefu ili baadaye Tanzania iwe na wataalamu nguli katika fani mbalimbali.
Madaktari wa Apollo
Umoja wa Hospitali ya Apollo una hazina kubwa ya ushirikiano na watu wa Tanzania.
Hospitali za Apollo zimetoa matibabu kwa watanzania kwa miaka kadhaa. Madaktari bingwa wa Hospitali za Apollo wamekuwa wakitembelea Tanzania mara kwa mara kwa ajili ya kutoa ujuzi wao wa kimatibabu kwa wagonjwa wa ndani ya nchi.
Madaktari bingwa wa Apollo pia wametoa mafunzo kwa madaktari wa Tanzania pamoja na wauguzi miaka michache iliyopita. Hii imewawezesha wafanyakazi wa hapa nchini kuchukua nafasi za kiufundi, muhimu na za usimamizi katika jamii.
Rais Kikwete alitembelea wagonjwa Watanzania waliolazwa katika Hospitali za Apollo pamoja na kuzungumza na familia za wagonjwa wanaopata matibabu katika hospitali hizo.
Historia ya Hospitali za Apollo
Mwaka 1983, Dk Prathap C Reddy, mbunifu wa afya nchini India, alianzisha hospitali ya kwanza.
Kwa miaka mingi, Hospitali za Apollo zimeendelea kukua na kuongezeka na sasa zimefanya kuwa moja ya shirika kubwa la afya barani Asia. Kwa sasa zipo zaidi ya hospitali 50 zenye vitanda  vipatavyo 8,500 na maduka 1,350 ya dawa na zaidi ya  kliniki za uchunguzi 100. 
Hospitali hizi  hutoa huduma za matibabu kwa utaratibu  wa kibiashara, huduma za bima za afya na Kitengo cha Tafiti za Kitabibu kwa lengo la kufanya tafiti za magonjwa ya milipuko, seli na maumbile.  Lengo ni kuendeleza vipaji ili kumudu hitaji linaloongezeka katika  utoaji wa huduma za hali ya juu. Mbali na huduma za tiba na tafiti, Hospitali za Apollo zina vyuo 11 vya madaktari pamoja na wauguzi. Hospitali na vyuo vyake vimekuwa katika nafasi ya juu kimataifa katika huduma za kitabibu pamoja na utafiti. 
Mpango wa NSSF kuleta nchini huduma za Hospitali za Apollo  ni mapinduzi yatakayoboresha sekta ya afya katika nyanja ya tiba, utafiti na teknolojia.
Ni mpango utakaowasaidia watanzania kupata huduma ndani ya nchi na kupunguza gharama  za matibabu  pamoja na safari za kwenda India.
Ni mipango ambayo siyo tu itapunguza gharama za kwenda kutibiwa nje ya nchi bali pia kuwapa uzoefu madaktari wa hapa nchini katika ujuzi wa tiba pamoja na teknolojia ya matumizi ya vifaa vya kisasa.
MWANANCHI