Wednesday, July 29, 2015

WATU 10 WAFARIKI KATIKA AJALI MBILI TOFAUATI




WATU 10 WAFARIKI KATIKA AJALI MBILI TOFAUATI

MAPADRI watatu na mtawa mmoja wa Kanisa Katoliki Jimbo la Rulenge wilayani Ngara walifariki dunia jana papo hapo huku watu 13 wakijeruhiwa katika ajali ya barabarani wakiwahi Karagwe kwenye misa ya shukrani ya mwenzao aliyepata daraja hilo hivi karibuni.


Tukio lingine ni la juzi ambapo watu saba walikufa na wengine 44 kujeruhiwa katika ajali iliyohusisha basi na treni ya mizigo mkoani Tabora. Ajali hiyo ya juzi watu wanne walikufa papo hapo huku wengine wakifia njiani wakipelekwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora, Kitete.
Katika tukio la kwanza la Ngara, kwa mujibu wa mmoja wa mapadri waliokuwa katika msafara huo, Erasto Nakule, ajali hiyo ilitokea jana saa 2:00 asubuhi katika barabara iendayo nchi jirani ya Uganda katika eneo la Bugorora wilayani Missenyi mkoani Kagera.
Alisema gari aina ya Land Cruser lenye namba ya usajili T.650 BY1 la Jimbo Katoliki la Rulenge lililokuwa likiendeshwa na Padri Florian Tuombe ambaye pia amefia katika Hospitali ya Mkoa Kagera liligongana uso kwa uso na basi la Kampuni ya Sabuni lenye namna ya usajili T.166 AGU.
Alisema basi la Sabuni lilikuwa likitoka wilayani Karagwe kwenda mkoani Mwanza, ambapo Land Cruser ilikuwa ikitoka Biharamulo kwenda Karagwe. Padri Nakule aliwataja mapadre waliofariki dunia katika ajali hiyo kuwa ni pamoja na Michael Mwelinde (70), Onesmo Buberwa (40) na Florian Tuombe aliyekuwa dereva na Mtawa Magreth Kadebe (60).
Hata hivyo, habari zaidi zinaeleza kuwa mapadri hao walikuwa ni walimu wa Seminari ya Rutabo wilayani Muleba na kwamba walikuwa wakienda kwenye misa ya shukrani ya Padre Evisius Shumbusho inayofanyika nyumbani kwao Karagwe.
Kamanda wa Polisi Mkoa Kagera, Augustine Ollomi alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kusema kuwa taarifa za awali zinaonesha kuwa chanzo chake ni dereva wa Land Cruser kuendesha bila kuchukua tahadhari hivyo kugongana uso kwa uso na basi la Sabuni.
Ajali ya Tabora Kutoka Tabora Lucas Raphael, anaripoti kwamba watu saba wamekufa na wengine 44 kujeruhiwa katika ajali iliyohusisha basi na treni ya mizigo mkoani hapa. Katika ajali hiyo iliyotokea juzi, watu wanne walikufa papo hapo huku wengine wakifia njiani na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora, Kitete.
Hayo yamethibitishwa na Kaimu Kamanda wa Polisi mkoa wa Tabora, Juma Bwire aliyesema basi lililogonga treni na kusababisha vifo na majeruhi ni mali ya Kampuni ya DonĂ¢€™t Worry lenye namba za usajili T 568 APB ambalo hufanya safari zake kati ya Tabora na Mabama wilayani Uyui.
Bwire aliwataja watu waliokufa kuwa ni Samwel Emmanuel (27) mkazi wa Ufuluma, Rehema Rashidi (45) mkazi wa Ugowola, Waziri Juma (32) mkazi wa Mabama, na Iddi Kionja (34) ambaye haijafahamika ni mkazi wa wapi.
Alisema chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva kwenda mwendo kasi na Jeshi la Polisi mkoani Tabora linamsaka dereva wa gari hilo ambaye alikimbia mara baada ya kusababisha ajali hiyo majira ya saa 7:40 mchana katika eneo la Malolo.
Treni hiyo ilikuwa inatoka Kigoma kwenda Tabora. Akizungumzia ajali hiyo, Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Mkaguzi wa Polisi, Michael Deleli alisema ajali hiyo imesababishwa na mwendo kasi wa basi kwani eneo ilipotokea ajali liko wazi mno kiasi kwamba hapakuwa na sababu yoyote ya kutokea ajali hiyo kama dereva angekuwa makini.
Alisema mazingira ya ajali hiyo ni kukosa umakini kwa dereva wa basi kwani alipokuwa amekaribia reli ghafla akaona treni inakuja mbele yake ndipo akaamua kukata kona kwa dharura lakini basi likamshinda na kudondokea kwenye njia ya treni kabla ya treni kuliburuza umbali kadhaa na kusababisha vifo na majeruhi hao.
Deleli alitoa wito kwa madereva wote hapa nchini kuwa makini wanapofika maeneo yenye makutano ya barabara na reli ikiwemo kuzingatia alama zilizoko barabarani wakati wote.
Aidha amelitaka Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) kuweka mageti na alama zinazoonekana kwenye maeneo hayo ya makutano au wasimamizi wenye bendera watakaoashiria ujio wa treni katika eneo husika.
Naye Mganga Mkuu Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Kitete, Dk Yussuf Bwire alithibitisha kupokea miili minne na majeruhi zaidi ya 44 na kwamba wengine wawili walifariki jana, muda mfupi baada ya kufikishwa hospitalini. Usiku wa kuamkia jana, majeruhi mwingine ambaye ni mwanafunzi wa shule ya Ndono, Paskazia Chimel (20) alifariki dunia.
Dk Bwire alisema majeruhi waliobaki hospitalini hapo ni wanawake 11,wanaume 9 na watoto 3 waliruhusiwa wawili na 21 waendelea vizuri na mwingine mmoja ambaye hajafahamika jina lake na hali yake ni mbaya