Serikali imetakiwa kuweka utaratibu utakaowezesha watoto yatima wanaoishi katika vituo mbalimbali nchini kusoma bila kubughudhiwa na walimu juu ya michango ambayo hukwamisha maendeleo yao.
Rai hiyo ilitolewa na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda (pichani), wakati wa uzinduzi wa kisima cha maji safi kilichotolewa msaada na Kampuni ya simu za mkononi ya Zantel kwa kituo cha watoto yatima cha Watoto Wetu Tanzania kilichopo Kimara Suka jijini Dar es Salaam. Pia Makonda aliahidi kuwasomesha watoto wanane waliokosa ada wanaolelewa katika kituo hicho pamoja na vijana watatu ambao wamemaliza kidato cha sita na kushindwa kuendelea na masomo yao kwa kukosa mkopo. Alisema mara nyingi kuongezeka kwa watoto wa mitaani kunatokana na mambo mbalimbali yakiwamo migogoro ya kifamilia, ndoa za utotoni pamoja na hali ya kipato kwa familia. Alisema familia ndiyo zenye jukumu la kumaliza tatizo la watoto wa mitaani kwa kuishi vizuri na watoto wao na kwa maadili kwani mara nyingi wao ndiyo chanzo kikubwa cha kuwapo kwa kundi hilo mitaani. "Ustawi wa watoto na vijana, ni jambo muhimu katika jamii, hivyo nakipongeza kituo hiki kwa kazi kubwa ya kulikumbuka kundi hili muhimu ndani ya jamii na kumaliza kero kubwa ya upatikanaji wa maji ambayo yamekuwa ni kero kubwa katika ukanda huu," alisema Makonda. Akizungumza katika halfa hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Pratap Ghose, alisema kampuni yake imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali za kusaidia maendeleo ya jamii na kiuchumi katika jamii inayowazunguka. "Mara kwa mara kampuni yetu imekuwa inalenga kugusa maisha ya wananchi wanaotuzunguka, na ndiyo maana tumeamua kutoa msaada huu wa kujenga kisima cha maji katika kituo hiki ili kisaidie na kumaliza matatizo yaliyokuwa yakiwakabili ya maji kwa muda mrefu," alisema Ghose. Kisima hicho kitakuwa na uwezo wa kuhudumia watoto zaidi ya 70 na kutatua changamoto ya muda mrefu ya shida ya maji safi na salama. Naye Mkuu wa kituo hicho, Evance Tegete, alisema kituo hicho hulea watoto kutoka kila sehemu kwani baadhi ya watoto wametoka nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Alisema tangu mwaka 1998 hadi sasa, kituo hicho kimesomesha watoto 386 bila kupata ufadhili kutoka serikalini. Alisema kuwa changamoto kubwa zilizopo katika kituo hicho ni kushindwa kuwalipia ada baadhi ya watoto pamoja na ukosefu wa rasilimali watu wa kudumu ambao watawahudumia watoto hao