Wakati mwingine migogoro ya ardhi inasababishwa na kutojua. Wengi hawajui taratatibu na ndio maana hujikuta wanainga katika matatizo. Moja ya maeneo ambako watu wamekuwa wakipatia matatizo ni huu wakati wa kununua. Yapo mambo mengi unapoununua ardhi, nyumba au kiwanja ambayo wewe kama mnunuzi unatakiwa kuyajua na kuyazingatia ili usiingie katika matatizo. Nimefanya utafiti katika kesi za ardhi mahakamani na kugundua kuwa moja ya eneo baya linalowaingiza watu mkenge ni hili la mume kuuza nyumba au kiwanja bila kupata ridhaa ya mke wake . Ikumbukwe kuwa suala la ridhaa hapa sio suala la hiyari isipokuwa ni suala la lazima na la kisheria ambalo kutolitekeleza kwake kunaweza kupelekea mnunuzi kupoteza kile alichokinunua. Ni hatari ndugu na umakini unahitajika.Mume anapouza nyumba/kiwanja kuna kitu huitwa ridhaa ya mwanandoa ambacho ni lazima akisaini, tutaona.
NINI MAANA YA RIDHAA YA MWANANDOA.
Ridhaa ya mwanandoa(Spouses consent) ni ridhaa ambayo anapaswa kuitoa mwanandoa inapokuwa inauzwa mali( nyumba/kiwanja/shamba) ambayo mwanandoa naye ana maslahi au anaimiliki kwa pamoja na mme wake au mke wake. Ridhaa hii pia huweza kutolewa na mume iwapo anayeuza ni mke na huweza kutolewa na mke iwapo anayeuza ni mume. Ni hatua ya lazima unapokuwa unanunua nyumba , kiwanja au shamba.
KWANINI MUHIMU ZAIDI MKE KUTOA RIDHAA.
Hapo juu tumeona kuwa pia mume anatakiwa kutoa ridhaa iwapo mke ndiye anayeuza halafu tukaona kuwa pia mke anatakiwa kutoa ridhaa iwapo mme ndiye anauza. Lakini utashangaa katika makala yangu naongelea zaidi mke kutoa ridhaa mume anapouza. Ninamuongelea mke kutoa ridhaa zaidi kwakuwa utafiti unaonesha kuwa migogoro mingi katika hatua hii imetokea baada ya mume kuuza bila ridhaa ya mke. Wanaume wengi ndio huwazunguka wake zao na kuuza.Hii ndio maana hata kichwa cha mada hii kinaongelea zaidi mume kuuza bila ridhaa ya mke kwakuwa hapa ndipo penye tatizo.
NI NYUMBA/KIWANJA GANI AMBACHO LAZIMA MUME KUPATA RIDHAA YA MKE.
Nyumba au kiwanja ambacho mume ni lazima kupata ridhaa ya mke ni ile ambayo wanaimiliki kwa pamoja. Wanayoimiliki kwa pamoja ni ile ambayo wamejenga kama wanandoa au kununua wakati wakiwa katika ndoa na ile ambayo mke wakati wa kuolewa amemkuta nayo mwanaume lakini wakati wakiwa wote katika ndoa kuna maendelezo yoyote waliyofanya hata yawe kiduchu. Kununua pamoja si lazima iwe huyu analeta hela na huyu analeta hela hapana hata kukaa nyumbani kupika, kufagia halafu mwanaume akatafuta hela na kununua ni kuipata pamoja na haiwezi kuuzwa bila ridhaa ya mke.
JE NYUMBA IKIWA KATIKA JINA LA MUME NI LAZIMA KUPATA RIDHAA YA MKE.
Ndio hata kama ipo katika jina la mume ni lazima kupata ridhaa ya mke. Nyumba au kiwanja kuwa katika jina la mume haiondoi matakwa ya sheria ya kuwa ni ya wote . Kuwa katika jina la mume ni taratibu tu lakini bado inakuwa ni ya familia au ya wote. Hapa wanaume huwalaghai wanunuzi kwa kuonesha majina yao kwenye hati ili wauze bila ridhaa ya wake. Mnunuzi usidanganywe na jina kwenye hati.
DOCUMENT YA RIDHAA YA MWANANDOA IWE NA VITU GANI.
Document ambayo inaitwa ridhaa ya mwanandoa ambayo wakati unauziwa kiwanja au nyumba ni lazima mke aisaini inakuwa na jina la mke wa muuzaji, ikieleza dini yake, anuani yake na ikiapa kuwa yeye ni mke halali wa muuzaji fulani fulani. Baada ya hapo kutakuwa na kipengele ambacho mwanamke ataapa kwa kutoa ridhaa yake ya kumruhusu mume wake kuuza nyumba au kiwanja na atakitaja hicho kiwanja/nyumba namba zake(plot no) na eneo kilipo ikiwa ni pamoja na kiasi cha mita kama ni kiwanja. Baada ya hapo atasaini kwa chini na kuandika jina lake na mume wake muuzaji ataandika jina lake naye atasaini.
NINI KITATOKEA MKE ASIPOSAINI DOCUMENT YA RIDHAA YA KUUZA NYUMBA/KIWANJA.
Ni rahisi tu kuwa unaponunua nyumba ambayo iko katika mazingira kama niliyoeleza bila mwananke kusaini ridhaa ya mwanandoa wewe mnunuzi unakuwa umepoteza kwakuwa ununuzi huo ni batili na mda wowote mke akiamua kurudisha ile nyumba anairudisha na mnunuzi unapata hasara.
UFANYE NINI MNUNUZI ILI KUEPUKA HILI.
Wanaume wengi ni wajanja na wanauza nyumba viwanja bila kujali hili na matatizo utayapata mnunuzi baadae. Na si rahisi mume akwambie ukweli kuhusu hili akishafanya maamuzi ya kuuza na hivyo usitegemee kumuuliza ili upate ukweli. La kufanya ni kuwa hakikisha unapepeleza kama muuzaji mume ana mke na ukijua ana mke hakikisha mwanamke anasaini hiyo document bila kujali ile mali inayouzwa ni yao wote au ya mume peke yake ili kuwa upande salama zaidi. Wewe mnunuzi huwezi kujua imepatikanaje hayo ni yao wanan doa yatakuchanganya. Sasa ili kuweka mambo sawa iwe yao wote au hapana we muombe tu muuzaji mke wake asaini nyaraka ya ridhaa kwakuwa kwa kufanya hivyo hapotezi lolote kama kweli hakuna jambo analoficha au kama hakuna utata. Narudia tena, usijaribu wala usinunue nymba au kiwanja kwa mume bila mke wake kusaini ridhaa ya mwanandoa utapata matatizo sana na ulichonunua ipo siku tu kitarudishwa na wewe utapoteza, ni hayo kwa leo.
MWANDISHI WA MAKALA HAYA NI MWANASHERIA NA MSHAURI WA SHERIA KUPITIA GAZETI LA SERIKALI LA HABARI LEO KILA JUMANNE, GAZETI JAMHURI KILA JUMANNE NA NIPASHE KILA JUMATANO.
0784482959, -0714047241 bashiryakub@ymail.com