Jana katika safu ya 'Ndani ya Habari' tulichapisha habari za uchunguzi zinazothibitisha kwamba kuna mtandao mkubwa ambao umeota mizizi katika mahakama zetu nchini.
Uchunguzi huo ulijikita hasa katika kufichua vitendo vya rushwa vinavyoendeshwa na mtandao huo katika baadhi ya mahakama hizo kutokana na ukweli kwamba waathirika wakubwa wa vitendo vya rushwa ni wananchi wa kawaida ambao kesi zao nyingi hupelekwa katika mahakama za mwanzo. Katika mahakama hizo, kuna mrundikano mkubwa wa kesi kutokana na kuwapo idadi ndogo ya mahakimu, lakini pia uchunguzi umegundua kwamba wananchi wengi wanaopeleka kesi au kufunguliwa mashtaka katika mahakama hizo ni maskini, hivyo hawana fedha za kutoa hongo kupitia mtandao huo.
Uchunguzi huo umejikita katika mahakama za mwanzo zilizoko jijini Dar es Salaam, baada ya kugundua kwamba mtandao wa rushwa katika mahakama hizo ni uleule uliopo katika mahakama zote nchini, kuanzia mahakama za chini hadi za juu. Jiji hili hubeba taswira ya kitaifa, kwa maana ya wakazi wake wengi kutoka katika mikoa yote nchini ikiwamo Visiwani. Hivyo, wengi wamesema kwamba mtandao wa mahakama za mwanzo jijini Dar es Salaam hakika ni kama ule uliopo katika mahakama za ngazi mbalimbali huko mikoani. Wamesema ni muhimu kumulika mahakama za chini kwa kuwa kesi nyingi zinazopelekwa katika mahakama hizo hatimaye huishia katika mahakama za juu baada ya kukatiwa rufani.
Ndiyo maana tumezimulika mahakama za mwanzo, tena za hapa jijini. Tumegundua kwamba mtandao wa rushwa umeathiri utoaji hukumu, utoaji haki na unachelewesha kesi kwa makusudi. Uchunguzi umebaini kwamba mtandao huo unasababisha ulaghai katika kuwapa dhamana watuhumiwa walioko mahabusu, huku wakati mwingine ikilazimisha kesi kumalizika kabla ya kutolewa hukumu. Ni mtandao hatari dhidi ya upatikanaji wa haki, hasa kwa watu walio wagumu kutoa rushwa ili kuwezesha kile kinachoitwa 'kusukuma kesi kwa mwendo wa kasi'.
Ni mtandao wa dhuluma ambao kwa kiasi fulani umeteka mifumo ya kimahakama na uendeshaji kesi, ambapo usumbufu unatengenezwa kwa walalamikaji, walalamikiwa na hata ndugu zao. Watu hao, kwa mfano, hulazimishwa kufika asubuhi sana mahakamani huku mtandao huo ukijua fika kwamba kesi zao zitasomwa jioni, kuahirishwa au kufutwa. Ni mitandao ya rushwa ambayo inawashirikisha baadhi ya wazee wa baraza, wanasheria feki, wanasheria halali, polisi, waendesha mashtaka na mahakimu.
Wapo washtakiwa ambao kesi zao zimekuwapo mahakamani kwa miaka mingi, lakini kesi hizo zimekuwa zikitajwa, huku wakiwa hawajawahi kupandishwa kizimbani. Kesi huahirishwa kwa visingizio mbalimbali, mara hakimu anaumwa, ana udhuru, mlalamikaji yupo safari, na kadhalika. Wakati wote huo wahusika huambiwa watoe kiasi fulani cha fedha, ingawa hata wakitoa fedha hizo, mitandao hiyo huendelea kuwalazimisha kufanya hivyo. Pengine ni kweli kwamba mtu wa kulaumiwa pia ni yule anayetoa rushwa, kama Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, John Kahyoza alivyomwambia mwandishi wetu katika mahojiano hivi karibuni. Hata hivyo, sisi tunadhani kwamba jambo muhimu na la haraka hivi sasa ni mamlaka husika kusimama kidete na kuusambaratisha mtandao huo, siyo tu katika mahakama za mwanzo, bali pia katika mahakama za ngazi zote hapa nchini. Lazima mamlaka hizo zitambue kwamba kufumbia macho vitendo vya rushwa katika baadhi ya mahakama zetu ni kuwanyima wananchi haki zao za msingi.
MWANANCHI.