WAZIRI Mkuu mstaafu wa Kenya, Raila Odinga amepongeza hatua za uimarishwaji wa uchumi na maendeleo uliofikiwa Zanzibar, hali ambayo imeendelea kuijengea hadhi na sifa kubwa Zanzibar katika kuimarisha sekta zake za maendeleo katika nchi za ukanda wa Afrika ya Mashariki.
Odinga alisema hatua hiyo, sio ngeni kwa Zanzibar, kwani imekuwa ikitambulikana kwa muda mrefu kutokana na historia yake kubwa ya kuimarisha sekta zake za maendeleo, ikiwemo biashara na nyinginezo kutokana na juhudi nzuri za viongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Alisema hayo jana Ikulu mjini hapa wakati akizungumza na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Ikulu na Utawala Bora), Dk Mwinyihaji Makame.
Odinga ambaye yuko Zanzibar kuhudhuria Mkutano wa Kuimarisha Masuala ya Ushirikiano katika amani, usalama na maendeleo kwa nchi za Afrika Mashariki, unaofanyika hapa Zanzibar chini ya Mwenyekiti wake, Rais mstaafu wa Zanzibar, Amani Abeid Karume.
Alisema kuwa Kenya inathamini uhusiano wa kihistoria uliopo kati yake na Zanzibar, tangu wakati wa ukoloni na kusisitiza kuwa wakati huo Zanzibar iliweza kutajirika kutokana na shughuli zake mbalimbali za kimaendeleo, ikiwemo biashara katika ukanda huu wa Afrika ya Mashariki jambo ambalo imeijengea sifa hadi hii leo.
Odinga alieleza kuwa kutokana na uhusiano sambamba na mafanikio yaliyopatikana kwa Zanzibar pamoja na nchi ya Kenya, kuna kila sababu ya kuendeleza uhusiano na ushirikiano wake huo wa kihistoria kwa manufaa ya pande zote mbili.
Alieleza kuwa anatambua umuhimu wa kuwepo uhusiano kati ya Kenya na Zanzibar na kusisitiza kuwa ipo haja kwa kuimarishwa zaidi mahusiano kwa nchi za Afrika ya Mashariki ili uchumi wa nchi hizo uzidi kuimarika zaidi.
Sambamba na hayo, Waziri Mkuu huyo alipongeza mafanikio makubwa yaliyopatikana katika kuendeleza, kuutunza na kuuthamini Muungano uliopo kati ya Tanganyika na Zanzibar.
Aidha, Odinga alisisitiza haja ya kuimarisha uhusiano na ushirikiano wa kibiashara na hata masuala ya ujasiriamali kati ya Kenya na Zanzibar kwa lengo la kuimarisha zaidi mashirikiano kati ya pande mbili hizo.
Dk Mwinyihaji alimpongeza Odinga kwa kuendelea kuthamini uhusiano na ushirikiano wa muda mrefu uliopo kati ya Kenya na Zanzibar; na kuendeleza utamaduni wake wa kuja kusalimiana na viongozi wa Zanzibar kila anapopata nafasi ya kufika Zanzibar.