Shirika linalosimamia safari za ndege nchini Kenya, KCAA, limetangaza kuwa anga ya Kenya itafungwa kwa muda wa dakika hamsini siku ya Ijumaa wiki hii ili kuruhusu ndege ya rais wa Marekani Barrack Obama kutua katika uwanja wa kimataifa wa ndege wa Jomo Kenyatta mjini Nairobi.
Kwa mujibu wa shirika hilo, agizo hilo litatekelezwa katika viwanja vyote vya ndege nchini Kenya na kuwa anga hiyo itafunguliwa muda tu pale ndege hiyo ya rais Obama itakapokuwa imetua.
Shirika hilo limesema kuwa limeyaandikia mashirika yote ya ndege na pia kampuni zote za usafiri kuhusiana na agizo hilo na kuwa safari za ndege kadhaa zitacheleweshwa siku hiyo na pia siku ya jumapili wakati rais Obama atakapokuwa akiondoka nchini Kenya kuelekea Ethiopia kwa muda wa dakika arubaini.
Awali idara ya polisi nchini Kenya ilikuwa imetangaza kuwa anga yote ya Kenya itafungwa kwa muda wa siku tatu kabla ya ziara hiyo lakini kwa mujibu wa shirika la KCAA ndege zote zinazopaa chini ya futi elfu ishirini hazitaruhusiwa kutua katika uwanja wa Jomo Kenyatta na uwanja wa wilson mjini Nairobi kuanzia siku ya Ijumaa hadi siku ya jumatatu, wakati wa kongamano la kimataifa ya ujasiriamali litakalofanyika mjini Nairobi.
Agizo hilo sasa linamaanisha ndege zote ndogo ndogo ambazo uhudumu kati ya Nairobi na Somalia na viwanja vingine vidogo vidogo katika kanda ya Afrika Mashariki, havitaruhusiwa kutua Nairobi hadi mkutano huo utakapomalizika.
Rais wa Marekani Barrack Obama anatarajiwa mjini Nairobi siku ya Ijumaa usiku ambapo anatarajiwa kuwa mwenyeji wa kongamano hilo la kibiashara kwa pamoja na mwenyeji wake rais uhuru Kenyatta.
Wakati huo huo, idara ya polisi nchini Kenya imetangaza ratiba ya usafiri wakati wa mkutano huo wa kimataifa.
Barabara kuu kati kati mwa mji mkuu wa Nairobi na zile zinazoelekea, katika makao makuu ya umoja wa mataifa mjini Nairobi zitafungwa wakati wa mkutano huo, na idara hiyo imetoa wito kwa Wakenya kujiepusha na shughuli katikati mwa mji na maeneo ya mkutano huo kuanzia siku ya ijumaa hadi siku ya jumapili.