Mgombea wa kiti cha urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe 'amefunguka' baada ya kupenya katika kundi la tano bora, akisema iwapo wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec), hawatamuunga mkono, yupo tayari kuheshimu maamuzi yao.
Membe na makada wenzake, Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Asha Rose Migiro, Naibu Waziri wa Sayansi, Mawasiliano na Teknolojia, January Makamba, Balozi wa Kudumu wa Umoja wa Afrika (AU), nchini Marekani, Amina Salum Ali, ndio waliopeta kati ya wagombea 38 waliorejesha fomu, wakiomba kuteuliwa na chama hicho kupeperusha bendera katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu.
"Hata kama sitachaguliwa na wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa, kuwa mgombea wa CCM katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu, nitamuunga mkono atakayechaguliwa. Kukubali kushindwa ni sehemu ya demokrasia na mimi nimejiandaa kisaikolojia kupokea matokeo yoyote…Lakini pia niwapongeze wote waliofika tano bora," alisema Membe.
MAGUFULI
Mgombea mwingine, Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli alipoulizwa kuhusu mapendekezo ya Kamati Kuu (CC) kuliteua jina lake kuwa miongoni mwa majina matano yatakayopigiwa kura ili kupata majina matatu yatakayopigiwa kura ili kumpata mgombea mmoja atakayepeperusha bendera yake dhidi ya vyama vya upinzani, alikataa kuzungumza huku akiwapungia mkono wananchi waliojitokeza eneo hilo.
MIGIRO
Naye, Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Asha-rose Migiro akizungumzia mchakato huo namna ulivyokwenda licha ya kuwapo kwa mpasuko kati ya baadhi ya wajumbe wa Kamati Kuu ambao wanapinga maamuzi ya kuminya wagombea wanaokubalika ndani na nje ya CCM akiwamo Lowassa, Migiro alisema kitendo cha kuaminiwa na CCM, hadi kufika hatua ya tano bora, ni unyenyekevu uliopitiliza ambao unapaswa kuheshimiwa."
MAKAMBA
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Sayansi, Mawasilino na Teknolojia, January Makamba, alisema "Tayari chama changu kinaamini kuwa mimi ninaweza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania...kwa hiyo kwangu mimi ni heshima kubwa sana."
NGELEJA
Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja ambaye ni miongoni mwa wagombea walioshindwa kupenya tabo bora, alisema kuwa kilichofanywa na Kamati Kuu ya CCM; ni utaratibu wa kawaida ambao vyama vilivyokomaa kidemokrasia vimekuwa vikiufuata.
"Mimi binafsi naafiki kuwa kilichofanyika ni utaratibu wa kawaida ambao hufuatwa na chama change. Wametenda haki wajumbe wa Kamati Kuu lakini pia nakubaliana nao kwamba, wagombea wote waliochaguliwa wana uwezo wa kuliongoza taifa hivyo sina wasiwasi nao,"