Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Uyui, Musa Ntimizi amefikishwa mahakamani kwa tuhuma za kumlawiti kijana mmoja (jina linahifadhiwa) mkazi wa Manispaa ya Tabora.
Mwenyekiti huyo alifikishwa mbele ya Hakimu Jocktan Rushwera na kusomewa mashtaka hayo, ikidaiwa na Wakili wa Serikali, Juma Masanja kuwa alitenda kosa hilo nyumbani kwake eneo la Bachu.
Mahakama ilielezwa kuwa mshtakiwa alimrubuni kijana huyo kwa kumnunulia bia mbili kwenye baa moja mjini Tabora kabla ya kutenda kosa hilo.
Wakili Masanja alidai kuwa baada ya kijana kulewa na kupoteza fahamu, mshtakiwa alimpeleka nyumbani kwake eneo la Bachu na kumlawiti.
Mshtakiwa alikana mashtaka na yupo nje kwa dhamana, Hakimu Ruchwera aliahirisha kesi hiyo hadi kesho itakapoanza kusikilizwa.
Wakati huohuo, polisi mkoani Simiyu wanamshikilia mkazi mmoja wa Kijiji cha Isenyi, Wilaya ya Serengeti mkoani Mara, kwa tuhuma za kukutwa na bunduki aina ya Rifle 375 yenye namba G 986189, ikiwa na risasi 10 kinyume na sheria.
Mtuhumiwa huyo ambaye anadaiwa kujihusisha na shughuli za uwindaji haramu kwenye hifadhi mbalimbali za Taifa, alikamatwa juzi saa 10 jioni katika Kitongoji cha Mwantimba, Kijiji cha Matondo, Tarafa ya Dutwa wilayani Bariadi.
Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Simiyu, Jonathan Shana alisema mtuhumiwa huyo baada ya kukamatwa aliongozana na askari kuwapeleka hadi Hifadhi ya Serengeti kuonyesha moja ya mabaki ya tembo, ambaye walimuua na kutoweka na meno yenye uzito wa kilo 36.
Shana alisema mtuhumiwa atafikishwa mahakamani baada ya uchunguzi kukamilika.
Hata hivyo, Shana alisema wanaendelea na msako kuwatafuta watu wanaojihusisha na ujangili wa wanyama pori, ambapo tangu Januari mwaka huu, tayari watu watano wameshakamatwa.