Mkurugenzi Msaidizi wa Habari, Elimu na Mawasiliano wa HESLB,
Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), imesema ilichelewa kutoa mikopo kwa wanafunzi wa vyuo vikuu nchini kutokana na sababu mbalimbali, zikiwamo kuchelewa kwa fedha kutoka serikalini, marejesho madogo ya mikopo na uchache wa fedha zilizokusanywa.
Akizungumza, Mkurugenzi Msaidizi wa Habari, Elimu na Mawasiliano wa HESLB, Cosmas Mwaisobwa, alisema HESLB ilishindwa kupeleka fedha kwa wakati kutokana na vyanzo vilivyotegemewa kutoa fedha kuchelewesha huku akisisitiza kuwa fedha iliyokwisha kusanywa haikuweza kutosheleza idadi ya wanafunzi wenye mahitaji.
"Siyo kama inavyoelezwa na vyombo vya habari, mikopo katika mihula yote ya kwanza ilitolewa kwa wakati, katika kipindi hiki cha muhula wa mwisho wa masomo mikopo imechelewa kwa sababu ya fedha zinazotengwa kwa ajili ya mikopo kuchelewa na urudishaji wa mikopo usioridhisha, alisema Mwaisobwa.
Aidha, alisema mikopo haikuchelewa kupelekwa katika vyuo vyote vyenye wanafunzi wenye mahitaji na kuongeza kuwa hata vyuo vilivyofanya migomo, baadhi ya vitivo vilikuwa vimepatiwa mikopo.
Alisisitiza kuwa HESLB imeshapeleka fedha za mikopo kwenye vyuo vyote na kuwa vyuo ambavyo wanafunzi hawajapokea, vina utaratibu wake wa kuwapatia fedha hizo.
Hivi karibuni, wanafunzi wa Vyuo Vikuu nchini vikiwamo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Chuo Kikuu cha Mtakatifu Joseph, Chuo Kikuu cha Iringa na Chuo Kikuu Kishiriki cha Ualimu cha Dar es Salaam (DUCE) waligomea masomo kuishinikiza serikali kupitia HESLB kuwapatia fedha za kujikimu.