Mamlaka ya Udhibiti Usafirishaji wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA), imewanoa wamiliki wa mabasi ya masafa marefu kuhusu usimamizi na udhibiti wa sekta ya usafiri wa barabara ili wazaidie kupunguza na kutokomeza kabisa ajali baada ya kuwapatia semina maalumu.
Semina hiyo maalumu ya siku mbili iliyoanza juzi mjini Morogoro imewashirikisha viongozi wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania ( TABOA) wakiongozwa na Mwenyekiti wao Taifa, Mohamed Hood, na kufunguliwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Dk Shaaban Mwinjaka.
Dk Mwinjaka katika hotuba yake ya ufunguzi, aliwataka wamiliki wa mabasi kuwatumia madereva wenye weledi ili kupunguza ajali ikiwa na hatua ya kuwaendeleza kielimu katika vyuo vya serikali na vya ufundi stadi Veta.
Mbali na hayo, aliwataka wamiliki wa mabasi kushirikiana na vyombo vingine kwa ajili ya kubaini mienendo ya madereva wao hasa suala la ulevi wanapokuwa kazini na mwendokasi, wakitambua mabasi yao wameyanunua kwa gharama kubwa na pia yamebeba uhai wa maisha ya binadamu.
Hata hivyo, alisema aliwahakikishia wamiliki wa mabasi ya masafa marefu kuwa, Kamati iliyopewa jukumu ya kuangalia namna ya kurekebisha sheria za makosa yanayowahusu wamiliki na kwa madereva wao imefikia hatua nzuri na muda si mrefu utawekwa hadharani.
Pamoja na hayo, pia aliwataka wamiliki wa mabasi kuhakikisha wanakuwa karibu kufuatilia kila jambo linalofanywa na dereva wake, kwani mwisho wa yote basi litabaki kuwa ni mali ya mmiliki na dereva ni mfanyakazi wake.
Naye Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini, Mohamed Mpinga alisema ajali za barabarani zinazohusisha mabasi hazitaweza kupungua iwapo sheria na kanuni za mwaka 2007 kanuni 317 hazitazingatiwa na wamiliki wa vyombo hivyo sambamba na madreva wao.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa SUMATRA, Gilliard Ngewe, mada sita ziliandaliwa na kutolewa kwa wamiliki wa mabasi ya masafa marefu, ikiwemo ya nafasi ya wamiliki wa vyombo vya usafiri katika kuimarisha usalama barabarani sambamba na nyingine ya kanuni ya taratibu za uwasilishaji makalamiko.