Wednesday, December 31, 2014

MTAALAMU WA VIUNGO NA MIFUPA AWASILI NCHINI


MTAALAMU WA VIUNGO NA MIFUPA AWASILI NCHINI
Mtaalam wa viungo na mifupa kutoka India, Dk. Shrirang Deodhar, anatarajiwa kuwasili nchini mapema baada ya Mwaka Mpya kwa ajili ya kuwafanyia uchunguzi na matibabu watu wanaosumbuliwa na maradhi hayo.


Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Hospitali ya Regency, Dk. Rajni Kanabar, mtaalam huyo ataendesha kambi ya siku tatu ya uchunguzi wa maradhi hayo katika hospitali hiyo Upanga jijini Dar es Salaam.
 
Alisema kambi hiyo ya uchunguzi imeratibiwa kwa pamoja baina ya Regency Medical Center na Klabu ya Lions ya Dar es Salaam Host.

Alisema uchunguzi huo utaanza Januari 4 hadi 6, mwaka huu kwenye hospitali hiyo na kutoa wito kwa watu mbalimbali wanaosumbuliwa na maradhi hayo kujitokeza kutumia fursa hiyo.
 
Alisema mtaalam huyo anatoka katika hospitali kubwa ya Shalby iliyoko mji wa Ahmedabad – Gujarat nchini India ambayo ni miongoni mwa hospitali kubwa ya mifupa nchini humo na barani Asia.
 
"Hii ni fursa ya pekee kwa Watanzania kuhudumiwa na mtaalam bingwa wa masuala ya mifupa na viungo… kwa wale wanaotaka ushauri na tiba, wanapaswa kutumia fursa kama hii kumuona mtaalam kwani kwenda hadi India kwa ajili hiyo kuna gharama kubwa sana," alisema Dk. Kanabar.
 
Alisema wagonjwa watakaokwenda kumuona mtaalam huyo, waende wakiwa na picha za X ray za hivi karibuni na ripoti za afya zao kwa ajili ya uchunguzi na ushauri wa kitaalam.
 
"Watu 200 wa kwanza ndiyo watakaopata fursa ya kumuona mtaalam, hivyo watu wenye matatizo kama haya wanapaswa kutumia nafasi hii adimu kumuona mtaalamu huyu," alisema.