Thursday, February 05, 2015

Siku 40 zakatika, albino aliyeibwa hajaonekana



Siku 40 zakatika, albino aliyeibwa hajaonekana
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Valentino Mlowola
Ni simanzi na majonzi katika kijiji cha Ndami, wilayani Kwimba ikiwa ni siku 40 sasa, tangu mtoto Pendo Emmanuel (4), atekwe na watu ambao hawajajulikana hadi sasa.
 
Mwenyekiti wa Kijiji hicho, Mwandu Madirisha, anasema wananchi wake hawapo vizuri kiakili tangu aibwe mtoto Pendo na kwamba "hawaamini kama mtoto yule hajaonekana mpaka leo."
 
Anasema kijiji hicho kina barabara kuu tatu zinazoingia na kutoka katika vitongoji vya Misasi, Nyahonge na Chibwiji, hali inayochangia kuwapo na ulinzi wa jadi (sungusungu).
 
"Hata hivyo, hawa sungusungu wanalinda katika njia zile kuu tu…siku ya tukio la kuibiwa mtoto 
 
Pendo, hakuna aliyefahamu wala kuhisi chochote kwani tumezoea kuishi kwa amani kwa miaka mingi," anasema.
 
Anasema kutokuwapo kwa matukio ya 'ajabu' katika kijiji hicho, ndiko kulikochangia watu wasio wema kutumia nafasi hiyo kumuiba Pendo na kutoweka naye kusikojulikana mpaka sasa. Madirisha anasema wakati watu hao wanatekeleza unyama wao kwa Pendo, kijiji kilikuwa hakina uongozi licha ya kuchaguliwa na wananchi, kutokana na kuchelewa kuapishwa mara baada ya kufanyika uchaguzi wa viongozi wa serikali za mitaa na vitongoji.
 
Mwenyekiti huyo anasema inawezekana watu hao walitumia hali hiyo kufanya 'uhalifu' wa kuvamia nyumba yao iliyopo mbali kidogo na barabara zinazolindwa na sungusungu.
 
"Naamini ni tukio la imani za kishirikina linalowahusu zaidi wafanyabiashara wa migodini pamoja na baadhi ya viongozi wa serikali ambao wanahitaji madaraka," anasema.
 
MAMA PENDO
Mama mzazi wa Pendo, Sophia Juma, ambaye kwa sasa amehamishwa katika makazi yake na kupelekwa wilayani Misungwi, hakuwa na mengi ya kusema kutokana na kumfikiria mtoto wake.
 
"Namkumbuka sana mwanangu, sielewi huko alipo kipi kimemtokea, lakini namwamini Mungu waliotenda jambo hilo, uso wa Mungu utawaumbua," anasema Sophia.
 
Anasema siku ya tukio akiwa na watoto wake wawili akiwamo Pendo, walilala chumbani na muda wa saa 4:00 usiku, walishitukia watu wameingia ndani na kumchukua mtoto kinguvu na kutoweka naye.
 
Hata hivyo, mama huyo hakuweza kuzungumza sana kutokana na simanzi alizonazo kuhusu mwanaye. 
 
MAJIRANI
Shigilu Kuya (70), ambaye nyumba yake ipo umbali wa mita 100 toka alipoibwa mtoto Pendo anasema alikuwa msibani wakati watekaji wanatimiza azma hiyo.
 
"Nilipokuwa msibani na mwanangu, usiku wa manane nilipigiwa simu na kuambiwa mtoto wa jirani Pendo amechukuliwa na watu wasiojulikana … nilishtuka na kuishiwa nguvu kabisa," anasema mzee Kuya.
 
"Nilikuwa namfahamu sana Pendo maana amekuwa akicheza hapa kwangu na wajukuu zangu, kutoonekana kwake kumetufanya tukose raha lakini tukiamini Mungu ipo siku watamuona tu," anasema.
 
Mzee Kuya anasema licha tukio hilo kushughulikiwa na kikosi kazi cha polisi, naye amefanikiwa kuisaidia polisi kwa kuwekwa mahabusu kutokana na tukio hilo.
 
Hata hivyo, anasema hafahamu kwa nini mtoto huyo ameibwa kwani hajawahi kusikia kijijini hapo kutokea kwa matukio kama hayo kwa miaka yake yote aliyoishi.
 
Kwa upande wake, Ngollo Maduka (50), jirani wa alipokuwa akiishi mtoto Pendo na wazazi wake, anasema anashikwa na hofu kubwa akimkumbuka mtoto huyo kutokana na jinsi walivyokuwa wakiishi naye na kucheza na wajukuu zake.
 
"Hatuamini kama tumempoteza Pendo, lakini naamini vyombo husika vitafanya kazi zake kiufasaha kuhakikisha wanafahamika na kufikishwa katika sheria wahusika wote wa tukio hilo bila upendeleo," anasema Ngollo.
 
VIONGOZI WA DINI
Mwinjilisti Hagai Mkumbo wa kanisa la AICT Ndami, kiongozi wa kanisa alilokuwa akiabudu mtoto Pendo na wazazi wake anasema:
 
"Pendo amekuwa mshirika wetu tangu wazazi wake wahamie hapa, tena walikuwa katika mafundisho ya ubatizo…tumehuzunika na kusikitishwa sana baada ya kusikia tukio hilo."
 
Anasema baada ya kupata taarifa ya watu kumuiba Pendo, kanisa lilifunga na kuomba kwa ajili yake ili Mungu asaidie kupatikana kwake, na wanaamini atapatikana.
 
Anasema wakati wa tukio hilo, baadhi ya waumini walienda nyumbani kwao kutoa msaada ingawa ilikuwa ngumu kuonana na mama yake kutokana na kuwapo na polisi wengi waliokuwa wakilinda eneo la nyumba yao.
 
Hata hivyo, anasema walipopata taarifa ya kuhamishwa mama Pendo nyumbani kwake, walifarijika na kumshukuru Mungu.
 
Mkumbo anasema tangu limetokea tukio hilo, limekuwa likiwaumiza na kuwakosesha amani, ingawa wanaamini Mungu ataingilia kati jambo hilo na kuweza kupatikana kwake.
 
David Mashimba ambaye ni mzee wa kanisa hilo, anasema walikuwa wakihitaji kupata mawazo ya Pendo na mama yake, lakini wamekosa hilo na kubaki kutafakari zaidi.
 
"Walikuwa wameanza mafundisho kwa ajili ya kubatizwa, lakini shetani amechukua nafasi yake kwa kuwaondoa katika nyumba ya Bwana," anasema Mashimba.
 
MKUU WA MKOA
Mkuu wa mkoa wa Mwanza, Magesa Mulongo, baada ya tukio hilo alitembelea kijiji cha Ndama kilichopo tarafa ya Mwamashimba wilaya ya Kwimba na kuzungumza na wananchi wake.
 
Mulongo alitaka kuwafahamu hatua iliyofikiwa na viongozi na wananchi katika kuwabaini waliotenda unyama huo kwa mtoto Pendo.
 
Anasema tukio hilo linasikitisha kwani halijawahi kutokea tangu 2007 wilayani humo wakati lilipomkumba mwananchi mmoja wa wilaya hiyo akisafiri kwenda mkoani Shinyanga kwa shughuli binafsi.
 
"Kiburi cha watekaji kimo humu humu haiwezekani mtu kutoka mbali aje atekeleze tukio kijijini bila yakuwa na wenyeji, lazima kuna mtu ama watu walioshirikiana na wahalifu hao. Mbona mifugo inapoibiwa hupatikana, iweje mtu asipatikane," anahoji Mulongo.
 
Hata hivyo, Mulongo pamoja na kutoa siku tano kwa waliofanya tukio hilo kupatikana, laini siku hizo zimeisha huku jeshi la polisi likiendelea kuwachunguza waliokamatwa kwa tuhuma hizo akiwamo baba mzazi wa Pendo, Emmanuel Shilinde.
 
MWENYEKITI WA ALBINO MWANZA
Mwenyekiti wa chama cha watu wenye ulemavu wa ngozi mkoani Mwanza, Alfred Kapole, amesema chama kinasikitisha kuona wanadamu wakiwaua wenzao kama wanyama na bila woga wowote.
 
"Inasikitisha kuona miongoni mwa kesi 72 zilizopo mahakamani, ni tatu tu ndizo zilizotolewa hukumu, lakini zingekuwa kesi ya wanasiasa kama wabunge wanashindana masuala ya uchaguzi wangetoa hukumu muda mrefu. Lakini si kwa walemavu wa ngozi," anasema Kapole.
 
Anasema hata kama wanadamu wanashindwa kutoa hukumu, Mungu atawahukumu na kutoa maandikio katika kitabu cha Biblia Takatifu, Mika 3.3-7, kinachoelezea hukumu watakayopata watu walao nyama za watu bila woga. 
 
Mwenyekiti Kapole amewaomba wasamaria wema wanaofahamu alipo Pendo wamrejeshe ama hata kama wamemdhuru basi mwili wake upatikane kwa ajili ya matanga na waliotenda jambo hilo wahukumiwe.
 
UNDER THE SAME SUN
Mkurugenzi mtendaji wa shirika la kuwalinda watu wenye ulemavu wa ngozi (albino), Under the Same Sun (UTSS), lenye makazi yake Canada, Peter Ash, ameshangazwa na vyombo vya dola kushindwa kuwakamata wanunuzi wa viungo vya albino licha ya kutajwa na waganga na wauaji.
 
Ash anasema viungo vya albino vinanunuliwa kwa bei kubwa ambayo mwananchi wa kawaida hawezi, lakini vyombo vya dola vinapowakamata wauaji na kuwahoji wanaelekezwa waliowatuma, bado vyombo vya dola vinashindwa kuwakamata.
 
"Inashangaza kuona licha ya kukamatwa kwa waganga ama wapiga ramli na wauaji wa albino, wakihojiwa na kuwataja wanaowauzia, wanashindwa kuwachukulia hatua…hali hii ni mbaya kwani bila jamii kusimama yenyewe 'mchezo' huo utanedelea," anasema Ash.
 
POLISI MWANZA
Awali akizungumza, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Valentino Mlowola, amesema kikosi kazi cha polisi kinaendelea na kazi ya upelelezi ili kuhakikisha waliotenda unyama huo wanapatikana.
 
"Tuliwakamata watu 15 akiwamo baba wa mtoto Pendo, Emmanuel Shilinde, lakini katika mchujo uliopitishwa ni watu wanane wanaoshikiliwa na jeshi hilo mpaka sasa," anasema Mlowola.
 
Anasema pia jeshi hilo limefanikiwa kuinasa pikipiki (bodaboda) iliyotumika kufanya unyama huo.
 
"Mlowola anasema licha ya kuendelea kuwahoji watu hao, lakini huo siyo mwisho kosa la jinai kutokana na kutokuwa na mwisho hata baada ya miaka 20 tukio hili litaendelea kuchunguzwa.
 
Aidha, amewataka wananchi kuendelea kufanya ushirikiano na polisi kwa kile wanachofahamu kuhusiana na kuibiwa Pendo huku akisisitiza jeshi lake likitangaza dau la Sh. milioni 3 kwa atakayefanikisha kupatikana kwake. 
 
Pendo ni miongoni mwa albino 74 waliopo wilayani Kwimba, huku akiwa namba tisa katika suala la kupatiwa ulinzi.
 
TAKWIMU
Takwimu za kimataifa zinaonyesha kuwa ni asilimia mbili  tu ya watu ambao huzaliwa na ulemavu wa ngozi ndiyo wanaosherehekea miaka 40 ya kuzaliwa kwao, huku takwimu hizo zikionyesha nchi za Afrika ni mtu mmoja kati ya 2,000 huzaliwa wakiwa albino wakati Marekani mtu mmoja kati ya 17,000 huzaliwa na ulemavu wa ngozi.
 
Mauaji ya albino nchini yanaonekana kukithiri zaidi katika mikoa ya Kanda ya Ziwa kutokana na imani za kishirikina, yakifuatiwa na mauaji ya vikongwe tangu yaliposhamiri mwaka 2006/07.