Wednesday, January 07, 2015

Taarifa Maalum ya IKULU Kuhusu Habari iliyochapishwa na Tanzania Daima



Taarifa Maalum ya IKULU Kuhusu Habari iliyochapishwa na Tanzania Daima

 

 Rais hajadharau Bunge

Gazeti la Tanzania Daima linalomilikiwa na Chama cha Upinzani cha CHADEMA
la leo, Jumapili, Januari 4, 2015, limeandika habari kwenye ukusara wake wa mbele chini ya kichwa cha habari: "Wabunge: Ikulu imetudhalilisha" hata kama wabunge wanaokaririwa katika habari hiyo ni wawili tu, Mheshimiwa Freeman Mbowe na Mheshimiwa David Kafulila.
Habari hiyo inadai kuwa Ikulu na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete kwa kuteua Mwenyekiti wa Bodi Mpya ya Wakurugenzi ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na kwa "kumruhusu" Waziri wa Nishati na Madini, Mhe. Sospeter Muhongo kuteua Wajumbe wapya wa Bodi hiyo, wamewadhalilisha Wabunge na "kuwafanya waonekana wajinga kwa sababu maamizio yao yametupwa."
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, inapenda kutoa ufafanuzi ufuatao
kuhusu madai hayo ya Waheshimiwa Mbowe na Kafulila:


(a) Kwamba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, kamwe hajapata kulidhalilisha Bunge ama Wabunge. Anafurahishwa na kazi yao nzuri na ushirikiano wao kwa Serikali yake. Rais Kikwete alirejea kusisitiza jambo hili majuzi tu na kulipongeza Bunge kwa kazi nzuri katika Salamu za Mwaka Mpya kwa Wananchi, Alhamisi iliyopita usiku.

(b) Kwamba uteuzi wa Mwenyekiti Mpya wa Bodi ya Wakurugenzi ya TANESCO, Profesa Mighanda Manyahi, uliofanywa na Mhe. Rais wiki iliyopita, unatokana na mamlaka aliyonayo kisheria na wala haukulenga kumdhalilisha yoyote, kama ambavyo teuzi nyingine nyingi azifanyazo, hazilenga kumfanya mtu yoyote *mjinga".

(c) Kwamba vile vile hadhi ya sasa ya Mhe. Muhongo, kama Waziri wa Nishati na Madini, bado inampa madaraka ya uteuzi kwa bodi zilizoko chini ya Wizara yake na wala hajapoteza "sifa ya kuendelea kuwa ofisini na hivyo kukosa sifa ya kuteua Wajumbe wa Wakurugenzi wa TANESCO"kama wanavyodai wabunge hao wawili.

(d) Kwamba uteuzi wa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TANESCO na Wajumbe wa bodi hiyo ni ushahidi mwingine usiopingika wa utekelezaji thabiti wa Maamizio ya Bunge lililojadili suala zima la Akaunti ya Escrow ya Tegeta na ushauri wa Bunge hilo kwa Mhe. Rais. Kumshtumu Mhe. Rais kwa hatua yake ya kutekeleza ushauri wa Bunge ni jambo la kushangaza sana.

(e) Kwamba, tofauti na baadhi ya shutuma za wabunge wa upinzani, Mhe. Rais ametekeleza kikamilifu kabisa ushauri uliotolewa kwake na Bunge katika maamizio yote manane, moja baada ya nyingine, ukiwemo ushauri kuhusu Bodi ya Wakurugenzi ya TANESCO na kuwajibishwa kwa maofisa mbali wa umma na waandamizi wa Serikali.

(f) Kwamba Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, inapenda kuwashauri Waheshimiwa Mbowe na Kafulila wakubali kufuata misingi ya haki ya kibinadamu katika kushughulika na watu wengine.

(g) Kwamba waheshimiwa hao hawawezi wao kuwa wapigaji mbinja (whistle blowers), wakawa wachunguzi, wakawa na mamlaka ya kukamata watu, wakawa na madaraka ya kushitaki, wakawa na madaraka la kuhukumu na wakawa na madaraka la kuwafikisha watu na jela na kuendelea kuwalinda huko. 
 
Tayari wamefanya kazi yao, tena vizuri sana Bungeni, sasa waachie watu wengine na vyombo vingine vilivyopewa mamlaka na madaraka kutekeleza yale yaliyoazimiwa Bungeni na kutolewa kama ushauri kwa Mhe. Rais. Aidha,
utekelezaji huo wa masuala ya umma unapokuwa hauendi kwa mujibu wa matakwa yao, pia wawe tayari kukubali kwa sababu katika demokrasia nzuri kama yetu na utawala bora safi kama wa kwetu, hakuna atakayefanikiwa kupata kila kitu anachokitaka na kama anavyokitaka.