Kurithi ni njia ambayo ni ya zamani zaidi kuliko njia zote za upatikanaji wa ardhi. Kurithi kumeanza enzi za mababu mpaka leo kupo.
Mambo ya mirathi ni mambo yenye sheria zinazokinzana kwa kiasi kikubwa na hapa ndipo ndugu huwa wanashikana mashati kugombea mali za marehemu.
Sheria za mirathi kimsingi ni pana, tutazijadili siku za usoni, lakini kwa leo naomba uelewe kuwa mtu anaweza kupata ardhi kwa njia ya urithi ukiacha njia nyingine.
Kutokana na ugumu wa maisha, gharama za viwanja kupanda ndiyo maana watu wengine hawanunui ardhi wanasubiri wapendwa wao wafariki ili wapate fursa ya kurithi.
Kimsingi, sheria za ardhi zinatambua urithi. Kwa mfano, Sheria ya Ardhi ya Vijiji ya Mwaka 1999 kifungu cha 18 (1) h, mtu anaweza kupata ardhi kwa kurithi kwa wosia au bila wosia.
Kifungu cha 67 cha sheria ya usajili wa ardhi sura ya 334, inaeleza kuwa mtu anaweza kuomba kusajiliwa kama mmiliki wa ardhi endapo atakuwa msimamizi wa mirathi ya marehemu.
Hakuna mtu anayepaswa kuanza kugawa mali za marehemu ikiwa ni pamoja na ardhi, hata kama ni mke, ndugu au mtoto wa marehemu. Mtu pekee anayeweza kufanya hivyo ni msimamizi wa mirathi.
Kimsingi mtu anapofariki, wanandugu wanapaswa kukaa kikao na kupendekeza mtu au watu kuwa wasimamizi wa mirathi, au kama kuna wosia basi mtu aliyetajwa kwenye wosia kuendelea na shughuli yake kuiomba mahakama imthibitishe kama msimamizi wa mirathi kwa mujibu wa sheria za mirathi za dini au mila husika.
Msimamizi akishachaguliwa anapaswa kukusanya baadhi ya vitu kwa ajili ya kuomba mahakama imchague kama msimamizi wa mirathi.
Baadhi ya vitu hivyo ni pamoja na cheti cha kifo, barua ya utambulisho kutoka serikali za mitaa, muhtasari wa kikao uliosainiwa na wahudhuriaji, kisha atafungua jalada la ufunguzi wa kesi ya mirathi.
Mahakama itaangalia kama maombi ya uteuzi wa usimamizi wa mirathi yamekidhi vigezo, basi mahakama itamsikiliza mwombaji na kufanya uteuzi wa msimamizi wa mirathi ambaye atakuwa ni mbadala wa marehemu na kuwa na nguvu zote za kisheria.
Mtu akishachaguliwa na mahakama, anapaswa kugawa mali za marehemu kwa warithi kwa mujibu wa sheria. Ikiwa miongoni mwa mali kuna ardhi ambayo haijasajiliwa, basi watapewa warithi. Kama kuna ardhi iliyosajiliwa, msimamizi wa mirathi anapaswa kuwagawia kwa kufanya haya yafuatayo:
Kwanza, huyu mtu chini ya kifungu cha 67 cha sheria ya usajili ya ardhi, atajaza fomu maalumu kwa ajili ya kubadili hati kutoka jina la marehemu kuja jina lake na akiambatanisha na barua ya usimamizi wa mirathi. Baada ya hapo hati itawekwa jina lake.
Mbili, baada ya hati kuwa na jina la msimamizi wa mirathi ya marehemu, basi chini ya kifungu cha 68 cha sheria hiyo, msimamizi atajaza fomu maalumu na kuomba hati iandikwe jina la warithi au mrithi. Hapo atakuwa amemaliza shughuli yake na tayari mtu atakuwa amejipatia ardhi kwa njia ya kurithi. Makala ijayo tutaangazia kupata ardhi kwa njia ya zawadi
Mwandishi wa Makala haya ni Jebra Kambole Wakili wa Kujitegemea kutoka Kampuni ya Law Guards Advocates wa jijini Dar es Salaam na Iringa.