Na mwandishi wetu
KERO ya maji safi na salama katika Shule ya Sekondari ya Nduguti wilayani Mkalama, mkoani Singida, imeanza kupatiwa ufumbuzi baada ya Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa huo Mhe. Martha Mlata, kubeba jukumu la kusaidia.
Mhe Mlata, ambaye amekuwa akishiriki kwenye kusaidia huduma za kijamii kuhususan elimu na afya, ametosa sh. Milioni tatu katika kuhakikisha kero hiyo inapatiwa ufumbuzi.
Awali, wanafunzi walikuwa wakilazimika kukatisha masomo kwa saa 40 kwa mwezi ili kufuata maji umbali mrefu hivyo kukosa masomo.
Akizungumza kwenye mahafali ya Sita ya Shule hiyo ambapo mgeni rasmi alikuwa Martha, Mkuu wa Shule Frank Malile, alisema tatizo la maji limekuwa sugu shuleni hapo.
Hata hivyo, alipongeza msaada huo wa Martha akisema utasaidia kupunguza kero hiyo na kwamba, ni mwanga wa kuelekea kwenye mafanikio ya kero hiyo kubaki historia.
"Shule yetu inakabiliwa na tatizo sugu la maji ambalo hukwmisha shughuli ikiwemo chakula kwa wanafunzi. Maji hufuatwa umbali mrefu na baadhi ya visima yanapopatikana ni vya wazi hivyo kuhatarisha usalama wa wanafunzi wetu," alisema.
Changamoto nyingine iliyowasilishwa mbele ya Martha ni uhaba wa nyumba za walimu, mabweni ya wanafunzi kutokuwa na madirisha, vitanda, vyoo na ukosefu wa jengo la utawala.
Akizungumza kabla ya kukabidhi vyeti kwa wahitimu, Martha alisema nyumba za walimu pamoja na umaliziaji wa majengo ya bweni la wanafunzi wa kike, nguvu za kila mzazi na mlezi zinahitajika.
Pia aliahidi kuwasiliana na uongozi wa Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA), ambayo imejikita zaidi kuhakikisha mabweni kwa ajili ya wanafunzi wakiwemo wa kike yanajengwa katika shule mbalimbali nchini.
Martha alisema TEA imeonyesha nia ya dhati ya kuanza kujenga mabweni 30 kwa ajili ya wanafunzi wa kike, ambao ni wahanga wa vitendo viovu katika jamii.
"Serikali imeamua kulivalia njuga suala hili kukomboa mtoto wa kike kutokana na vikwazo anavyopata katika elimu vikiwemo mila potofu kuwatumia watoto wa kike kama chombo duni kisicho na msaada.
Katika mahafali hayo, mbali na kukabidhi sh. Milioni tatu taslim mbunge huyo, miti 50 ya miembe kwa ajili ya kuimarisha mazingira, vifaa vya michezo kwa shule za wanawake na wanaume.
Pia, alikabidhi sola 19 ambazo zitasambazwa kwenye sekondari za kata kwa ajili ya kuwezesha wanafunzi kusoma nyakati za usiku.