Nuru Mwasampeta na 
        Veronica Simba, Dar es                Salaam 
        Waziri wa Nishati na                Madini, Profesa Sospeter Muhongo amesema Wizara yake                imejipanga kuhakikisha inajengwa mitambo ya uchakataji                madini (Mineral Processing Plants) hapa nchini ili                kuondokana na utaratibu wa kusafirisha madini ghafi nje ya                nchi na badala yake zisafirishwe bidhaa zitokanazo na                madini husika ili kuongeza thamani na hivyo kukuza pato la                nchi. 
         Aliyasema hayo                 alipokutana na kuzungumza na Wawekezaji wa Kampuni ya                Chinalco ya nchini China waliokuja nchini kwa lengo la                kujadiliana na Viongozi Waandamizi wa Wizara kuhusu fursa                za uwekezaji hususan katika sekta ya madini. 
        "Tunahitaji kuwa na                mitambo ya uchakataji madini hapa nchini hivyo nawashauri                katika uwekezaji wenu mfikirie suala la kujenga mtambo                husika kwani hatutaki kusafirisha madini ghafi nje ya                nchi," alisisitiza Profesa Muhongo.
         Katika mazungumzo hayo,                Waziri Muhongo aliwashauri wawekezaji hao ambao                walioambatana na Balozi wa China nchini, Mhe. Lu Youqing                kuhusu fursa muhimu za uwekezaji katika sekta ya madini                hapa nchini kuwa ni uwekezaji katika madini yaliyo katika                kundi adimu (Rare Earth Elements), madini ya Shaba                (Copper) pamoja na madini ya Dhahabu. 
        Aliwashauri wawekezaji                hao kukutana na Wataalamu kutoka Shirika la Madini la                Taifa (Stamico) ambalo limepewa dhamana ya kusimamia                maeneo yote ya uwekezaji katika sekta ya madini kwa niaba                ya Serikali, ili kujadiliana kuhusu uwezekano wa kuingia                ubia katika uwekezaji husika ikiwa ni pamoja na kupata                maelezo ya kina kuhusiana na uwekezaji katika sekta ya                madini. 
        Kwa upande wake, Katibu                Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi                aliwaeleza wawekezaji hao kuwa Tanzania inajulikana vizuri                kwa kuwa na mazingira mazuri ya kijiolojia yanayofaa kwa                uwekezaji hususan kwa madini kama dhahabu, vito, shaba,                nickel na cobalt na kwamba aina ya miamba inayopatikana                nchini inaruhusu madini ya aina nyingi kupatikana akitolea                mfano Tanzanite ambayo inapatikana Tanzania pekee. 
         Aidha, aliongeza kuwa                Tanzania inayo sera nzuri ya madini, utawala bora, hali                nzuri ya kisiasa (political stability) pamoja na                miundombinu bora, ambazo ni miongoni mwa sababu za msingi                zinazovutia uwekezaji nchini. Naye Kamishna wa Madini,                Mhandisi Paul Masanja aliwakaribisha wawekezaji wa Kampuni                ya Chinalco kuja kuwekeza nchini na aliahidi kuwapa msaada                utakaohitajika ili kufanikisha azma yao hiyo ikiwa ni                pamoja na kuwapa leseni ya kutafuta au kuchimba madini kwa                wakati. 
        Awali, Mwenyekiti wa                Kampuni ya Chinalco, Bw. Xiong Weiping akiinadi Kampuni                yake kwa Viongozi wa Wizara alieleza kuwa, Kampuni hiyo ni                mali ya Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China na                inasimamiwa na Serikali Kuu na kwamba inajihusisha na                masuala ya maendeleo ya rasilimali za madini, uchakataji                wa madini ghafi na masuala ya kiufundi (technical &                engineering services). 
        Alisema mkakati wa                kampuni hiyo ni kuendelea kupanua shughuli za uzalishaji                wa madini ya Aluminum, Shaba, Rare Earth Element na                uongezaji thamani madini. Ziara ya Kampuni hiyo nchini                imekuja kufuatia ziara zilizofanywa awali nchini China kwa                nyakati tofauti na Mhe. Waziri Mkuu wa Tanzania, Mizengo                Pinda na Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM),                Abdulrahman Kinana katika Makao Makuu ya kampuni hiyo                mapema mwaka jana na kuuomba uongozi wa kampuni hiyo                kupanua mipaka ya biashara hadi Tanzania. 
                Waziri wa Nishati na                Madini, Profesa Sospeter Muhongo akiongea na Wawekezaji                wa Kampuni ya Chinalco ya nchini China waliokuja nchini                kwa lengo la kujadiliana na Viongozi Waandamizi wa Wizara                kuhusu fursa za uwekezaji hususan katika sekta ya madini. 
                Wawekezaji wa Kampuni ya                Chinalco ya nchini China wakiongea na Waziri Muhongo
                 Katibu Mkuu wa Wizara                ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi katika picha na                waekezaji hao pamoja na maofisa wa wizara
        .jpg)
.jpg)
.jpg)