
Na Profesa Mbele
        Leo nimepata zawadi                  ya kitabu, Picturing                  Hemingway's Michigankilichotungwa                  na Michael R. Federspiel. Kinahusu sehemu ya kaskazini                  ya jimbo la Michigan, ambapo familia ya Ernest Hemingway                  ilikuwa inakwenda kwa mapumziko. 
        Kitabu kina picha na                  maelezo kuhusu sehemu hiyo, ambapo Hemingway alitembelea                  tena na tena wakati wa utoto na ujana wake. Hapa ni                  chimbuko la matukio ya riwaya ya mwanzo ya Hemingway,The                  Torrents of Spring na hadithi zake ziitwazo Nick Adams                  Stories. 
                Nimeletewa kitabu hiki                  na Bwana David Cooper wa Ohio na mwanae Clay ambaye ni                  mwanafunzi wangu aliyekuja Tanzania mwezi Januari, 2013                  katika kozi yangu ya "Hemingway in East Africa."
                Baba huyu ndiye                  aliyetupeleka Montana kwa ndege yake mwaka jana,kuonana                    na Mzee Patrick Hemingway. Hapa kushoto ni picha                  tuliyopiga mjini Lakeville, Minnesota, kabla ya kuruka                  kwenda Montana. Bwana Cooper anaonekana kulia kabisa,                  halafu anafuata mwanae, halafu mwanafunzi wangu mwingine                  aliyekuwemo katika kozi ya "Hemingway in East Africa,"                  na mimi naonekana kushoto kabisa.
                Mwanafunzi                  aliyeniletea kitabu anaonekana nami pichani hapa                  kushoto, tukiwa kwenye mpaka baina ya hifadhi za                  Ngorongoro na Serengeti.
        Nilipokipata kitabu                  hiki, yapata saa saba mchana, nilijawa na furaha,                  nikaanza kukisoma mara, lakini nikaona nipige kwanza                  simu kwa walioniletea. Nilimpata Bwana Cooper,                  nikamshukuru sana. Ameniambia kuwa yeye na mwanae                  walikiona kitabu hiki katika duka kule sehemu ya                  Michigan Kaskazini, wakaniwazia. Baada ya maongezi                  nimeendelea kukisoma, nikamaliza baada ya masaa mawili                  hivi.. 
                Wameninunulia nakala                  yenye sahihi ya mwandishi, kama inavyoonekana hapa                  kushoto. (Ninaposema hivi, mawazo yangu yameshakwenda                  kwenye mazungumzo baina yangu na Ndugu Christian Bwaya                  kuhusu suala hili la kusainiwa vitabu).
        Nilifahamu kuwa sehemu                  hii ya Michigan Kaskazini ni muhimu katika utoto na                  ujana wa Hemingway, lakini kitabu hiki kimenifungua                  macho zaidi kwa kuonyesha sehemu mbali kwa picha na                  maelezo. Picha nyingi ni za mtoto Hemingway na watoto                  wengine katika familia yao, picha za wanaukoo, na sehemu                  mbali mbali. Nyingi katika ya picha hizo sikuwa                  nimeziona kabla. Kwa yote hayo, nimefurahi sana.