Na Asteria Muhozya, Dar es Salaam
Naibu Waziri wa Nishati na Madini anayeshughulikia Madini, Stephen Masele amesema kuwa bara la Afrika linahitaji taaluma ya sayansi kutokana na umuhimu wake kwa maendeleo na ukuaji wa uchumi. Masele ameyasema hayo jijini Dare es Salaam wakati akifunga Mkutano wa Tatu wa Vijana Wanasayansi Duniani (YES), na kuongeza kuwa, Afrika inahitaji sayansi kwa ajili ya kufanya ugunduzi na tafiti ambazo zitachangia katika kuchochea maendeleo barani Afrika.
Aliongeza kuwa, kutokana na umuhimu huo, Wizara ya Nishati na Madini imedhamiria kuwekeza kwa vijana katika tasnia ya sayansi ikiwemo kuhamasisha Vyuo Vikuu nchini, kuanzisha masomo ya sayansi hususan katika sekta ndogo ya gesi na mafuta jambo ambalo litawezesha kuzalisha wataalam wengi zaidi watakaosaidia kuendeleza taaluma hiyo na rasilimali zilizopo nchini.
Kutokana na umuhimu huo, aliutaka Mtandao wa Vijana Wanasayansi Duniani (YES), kuhakakikisha unasaidia kuwezesha vijana kuona umuhimu wa kuingia katika taaluma ya sayansi hususan jiolojia ili kuwezesha bara la Afrika kuwa na wataalamu wengi watakaosaidia kuharakisha maendeleo kupitia rasilimali asilia.
"Mtandao wa vijana mna jukumu la kuchochea taaluma ya sayansi kwa vijana. Afrika inahitaji wanasayansi wakutosha, kwa kuwa, uwepo wao utasaidia kuchochea ukuaji wa viwanda na teknolojia barani Afrika," alisisitiza Masele.
Aidha, alieleza kuwa, Afrika inahitaji wataalamu wanasayansi hivyo, alitoa wito kwa kuwashirikisha vijana katika masuala ya kitaaluma ikiwemo kufanya maamuzi.
"Nikiwa kiongozi kijana, nawataka vijana kuona umuhimu wa taaluma hii, hivyo, nawatanguliza ninyi katika hili, nendeni mkawafundishe na kuwahamasisha wenzenu waone umuhimu wa sayansi kwa dunia na kwa Afrika,"alibainisha Masele.
Aidha, aliongeza kuwa, kama kiongozi kijana, atatumia nafasi yake, kusaidia uwepo wa sera nzuri ambazo zitahamasisha ukuaji wa taaluma ya sayansi na kuwezesha vijana kisayansi.
Kwa upande wake, Rais wa Vijana Wanasayansi Duniani, Meng Wang alieleza kuwa, mkutano huo wa tatu umeacha historia kwa Tanzania na Afrika kutokana na kupata nafasi ya kukutana, kujadili na wanasayansi wakubwa waliobobea katika masuala ya Jiolojia Afrika na Duniani jambo ambalo litasaidia kuchochea ari ya vijana kuendeleza taaluma hiyo ikiwa ni pamoja na kuhamasisha vijana wengi zaidi kuingia katika sekta hiyo.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini anayeshughulikia Madini, Mhe. Stephen Masele akizungumza wakati akifunga Mkutano wa Tatu wa Vijana Wanasayansi Duniani, jijiji Dar es Salaam.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini anayeshughulikia Madini, Mhe. mStephen Masele akimpa zawadi ya kinyago iliyotolewa na mtandao wa Vijana Wanasayansi Duniani (YES), Rais wa Wajilojia barani Afrika Profesa Aberra Mogessie.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini anayeshughulikia Nishati, Mhe Stephen Masele, katika picha ya pamoja na baadhi ya Wanasayansi Vijana Duniani waliohudhuria mkutano tatu nchini Tanzania. Wengine katika picha waliokaa kutoka kushoto ni Mtendaji Mkuu Wakala wa Jiolojia Tanzania, Profesa Abdulkarim Mruma, Rais wa Wajilojia Barani Afrika Profesa Aberra Mogessie, Rais wa Vijana Wanasayansi Duniani Meng Wang na Mwenyekiti wa Vijana Wanasayansi, Tanzania Steven Nyagonda.