Mtoto wa Kitanzania,                msichana Neema Steven Mtwanga, ameibuka kinara katika                Mashindano ya Utunzi wa Insha katika nchi wanachama wa                Jumuia ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) kwa                kushika nafasi ya kwanza miongoni mwa washindani 39                waliowania Tuzo ya Utunzi wa Insha hiyo kwa Mwaka 2014. 
        Msichana Neema Steven                Mtwanga, 16, kutoka Shule ya Sekondari ya Naboti, Mkoa wa                Njombe, ametunukiwa Tuzo ya ushindi huo katika Mkutano wa                34 wa Kawaida wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa SADC ulioanza                leo katika Hoteli ya Elephant Hills Resort, Victoria                Falls, Zimbabwe. 
        Nafasi ya pili imeshikwa                na Kudzai Ncube kutoka Shule ya Sekondari ya Mazowe nchini                Zimbabwe na nafasi ya tatu imeshikwa na Manxoba Msibi                kutoka Shule ya Sekondari ya Etjendlovu katika Swaziland. 
        Kwa ushindi huo, Neema                Steven Mtwanga ambaye yuko kidato cha nne, amezawadiwa                hundi ya dola za Marekani 1500 ambayo ni sawa na shilingi                milioni 2.3 na amelipiwa gharama zote za kumwezesha                kushiriki katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi za SADC na                kukabidhiwa zawadi hiyo. Aidha, Neema amepewa zawadi ya                ipad kwa ajili ya matumizi yake ya teknolojia ya                mawasiliano na habari. 
        Mashindano hayo ya Insha                ya Mwaka 2014 yalianzishwa rasmi Oktoba, 2013 ambako                washindani walitakiwa kuandika Insha kuhusu mada: "Climate                Change is having adverse effect on the socio-economic                development in the Region. What should the Education                Sector do to mitigate the impact on the youth" –                Mabadiliko ya Tabia Nchi yanaathiri maendeleo ya kijamii                na kiuchumi ya Kanda ya SADC. Nini Sekta ya Elimu ifanye                kupunguza athari hizo kwa vijana? 
        Insha 39 zilipokelewa                kutoka nchi 13 kati ya nchi 15 wanachama wa SADC ikiwa ni                Insha tatu kwa kila nchi. Insha zilipokelewa kutoka                Tanzania, Angola, Botswana, Jamhuri ya Kidemokrasia ya                Congo (DRC), Lesotho, Malawi, Mauritius, Mozambique,                Namibia, Afrika Kusini, Swaziland, Zambia na Zimbabwe. 
        Majaji wa kupitia na                kuamua washindi wa Insha hizo walitoka Tanzania, Zambia na                Zimbabwe na walikutana mjini Gaborone, Botswana, Julai,                mwaka huu kupitia Insha zote na kutoa uamuzi wa nani                washindi. Ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano huo wa SADC                umepokea kwa furaha ushindi wa msichana Neema ukieleza                kuwa ushindi huo umeiletea Tanzania heshima kubwa katika                eneo la SADC na nje ya eneo hilo. 
        Imetolewa na; 
        Kurugenzi ya Mawasiliano                ya Rais, 
        Ikulu – Dar es Salaam. 
        17 Agosti,2014 
                        Rais Dkt.Jakaya Mrisho                Kikwete akimpongeza mwanafunzi wa kidato cha nne Neema                Steven Mtwanga(16) anayesoma katika shule ya sekondari                Naboti Makambako,Njombe baada ya kuibuka mshindi wa kwanza                katika utunzi wa insha katika shindano lililoandaliwa na                Jumuiya ya uchumi ya maendeleo kusini mwa                Afrika(SADC).Rais Kikwete alimpongeza mwanafunzi huyo                wakati wa hafla ya ufunguzi wa mkutano wa 34 wa wakuu wa                nchi za SADC unaofanyika katika mji wa kitalii wa Victoria                Falls, nchini Zimbabwe ambapo mwanafunzi huyo aliandika                insha inayohusu mabadiliko ya tabia nchi.
                        Rais Dkt.Jakaya Mrisho                Kikwete(kulia) akiwa katika picha ya pamoja na wakuu na                wawakilishi wa nchi za Jumuiya ya uchumi kusini mwa Afrika                SADC muda mfupi baada ya ufunguzi wa mkutano wa 34 wa                jumuiya hiyo uliofanyika katika hoteli ya Elephant Hills                mjini Victoria Falls Zimbabwe leo.Katikati ji mwenyeji wa                Mkutano huo Rais Robert Mugabe na  Dkt Stergomena Tax [katibu mkuu wa SADC] na                  kwa upande wake wa kushoto ni Nkosazana Dlamini-Zuma                   (Mkuu wa Tume ya Umoja wa Afrika)
                                    
        
        


 
