Aidha, SADC imemshukuru na kumpongeza                  aliyekuwa Katibu Mtendaji wa Kamati ya Ukombozi ya                  Afrika, Brigedia Hashim Mbita wa Tanzania, kwa mchango                  wake na uongozi wake wa mapambano ya ukombozi, iwe                  katika nyanja ya kuviwezesha vyama vya ukombozi kwa hali                  na mali, raslimali na ushauri.
        Pongezi hizo kwa Tanzania zilitolewa                  usiku wa jana, Jumamosi, Agosti 16, 2014, na Kikao cha                  Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC – SADC                  Troika- kilichofanyika kwenye Hoteli ya Elephant Hills                  Resort, Victoria Falls, Zimbabwe, chini ya Uenyekiti wa                  Rais Hifikepunye Phohaba wa Namibia.
        Mkutano huo wa SADC Troika                  ulihudhuriwa na wanachama wa Asasi hiyo – nchi za                  Namibia, Lesotho na Tanzania. Nchi za Afrika Kusini,                  Madagascar na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC)                  zilishiriki kama waalikwa maalum wa kikao hicho.
        Akizungumza kwenye mkutano huo kwa                  niaba ya nwenzake, Rais Pohamba alisema: "Tunawashukuru                  wananchi wa Tanzania kwa mchango wao wa kiuchumi,                  kijeshi na kimkakati katika kuunga mkono kwa hali na                  mali jitihada za mapambano ya ukombozi wa nchi zetu."
        Aliongeza Rais Pohamba: "Sote                  tunaijua Tanzania, sote tunawajua Watanzania.  Kwa                  pamoja walitoa jasho na damu na sisi wenyewe katika                  kutafuta ukombozi wa nchi zetu. Tutaendelea kukumbuka na                  kuenzi mchango wao mkubwa na usiosahaulika kwa ustawi wa                  nchi zetu."
        Kuhusu Mzee Mbita, ambaye Ripoti yake                  ya shughuli za ukombozi ilitarajiwa kuwasilishwa kwenye                  Mkutano wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa SADC, Rais Pohamba                  alisema: "Brigedia Mbita alifanya kazi mchana na usiku                  kufanikisha shughuli za ukombozi wa Kusini mwa Afrika.                  Tunamshukuru sana kwa uongozi wake na mchango wake                  mkubwa katika kuleta uhuru wa nchi zetu."
        Aliongeza: "Brigedia Mbita ni raia wa                  Tanzania na alikuwa Katibu Mtendaji wa Kamati ya                  Ukombozi Kusini mwa Afrika iliyokuwa na makao makuu yake                  mjini Dar es Salaam. Alichapa kazi kweli kweli na chini                  ya uongozi wake, vyama vya ukombozi vilipata misaada ya                  hali na mali, misaada ya kiroho na ushauri wa kijeshi                  kwa sababu yeye mwenyewe alikuwa mtu wa shughuli za                  jeshi." Mzee Mbita aliongoza Kamati ya Ukombozi tokea                  mwaka 1974 hadi ilipomaliza shughuli zake.
        Akizungumza kwa ufupi sana katika                  kikao hicho, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,                  Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete alimpongeza sana                  Brigedia Mbita akisema kuwa alifanya kazi nzuri na kubwa                  na "tunampogeza kwa kazi nzuri sana ya kuandaa Ripoti                  hiyo."
        Ripoti hiyo inayojulikana kama Mradi                  wa Hashim Mbita iliongozwa na Meneja wa Mradi, Profesa                  Arnold Temu wa Tanzania na imechapishwa na Kampuni ya                  Mkuki na Nyota, pia ya Tanzania, ambayo Mtendaji Mkuu                  wake, Mzee Walter Bgoya ameandamana na mwakilishi wa                  Mzee Mbita kwenye mkutano huo.
        | Imetolewa na; Kurugenzi ya                          Mawasiliano ya Rais, Ikulu – Dar es Salaam. 17 Agosti,2014 | 
.jpg)
 
