Monday, August 18, 2014

Mke wa Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar mgeni rasmi kwenye hafla ya kuwaaga wanafunzi wa Zanzibar wanaosoma chuo Kikuu cha Kiislamu Morogoro



Mke wa Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar mgeni rasmi kwenye hafla ya kuwaaga wanafunzi wa Zanzibar wanaosoma chuo Kikuu cha Kiislamu Morogoro
Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mama Asha Suleiman Iddi alisema kwamba utitiri wa vyuo vikuu bila ya ubora wa elimu inayotolewa ni jambo linalopelekea vyuo hivyo kutoa vijana wasiouzika kiajira katika taasisi mbali mbali za umma na hata zile za binafsi.

Mama Asha Suleiman Iddi alisema hayo wakati wa hafla maalum ya kuagana kwa wana jumuiya ya wanafunzi wa Zanzibar wanaosoma chuo Kikuu cha Kiislamu Morogoro wa ZAMUMSA ambao wanatarajiwa kumaliza mafunzo yao mwezi Novemba mwaka huu iliyofanyika katika ukumbi wa Zamani wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar uliopo Kikwajuni Mjini Zanzibar.

Katika kuunga mkono jumuiya hiyo ya wanafunzi wa Zanzibar wanaosoma chuo kikuu cha Kiislamu Mkoani Morogoro Mke huyo wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mama Asha aliahidi kuipatia mchango wa Kompyuta, Printa na Mashine ya Fotokopi Jumuiya hiyo ili ipate nguvu zaidi za kiutendaji.

Hata hivyo Mama Asha aliwaasa na kuwatahadharisha wanafunzi hao wa elimu ya juu kujiepusha na ushawishi wa wanasiasa kwa kuwatumia kujiingiza katika matendo maovu ya uvunjifu wa amani ya Nchi.

Akisoma risala ya wanajumuiya hiyo ya Wanafunzi wa Zanzibar wanaosoma Chuo Kikuu cha Kiislamu Mkoani Morogoro { ZAMUMSA } Mwanajumuiya Saleh Haji alisema lengo la kuanzishwa kwa Jumuiya hiyo mwaka 2006 ni kuwaunganisha pamoja wanafunzi wote ili kuwa rahisi kukabiliana na changamoto wanazopambana nazo.

Mapema Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanafunzi wa Zanzibar wanaosoma chuo Kikuu cha Kiislamu Morogoro Hamad Ali alisema wanajumiya hao wameamua kujitolea kuitumikia nchi yao licha ya changamoto wanazopambana nazo.

Hamad Ali alisema wanafunzi hao wanahitaji kuitumia taaluma waliyojifunza kwa kuisaidia jamii iliyowazunguuka katika maeneo yao.
Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wanafunzi wa Zanzibar wanaosoma chuo kikuu cha Kiislamu Morogoro Nd.Kassimu N'gwali akitoa neno la shukrani kwa waalikwa wa hafla yao ya kuagana kwa wanajumiya wanaomaliza masomo yao mwezi Septemba mwaka huu wa 2014. Kulia ya Ndugu N'gwali ni Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ambae ndie mgeni rasmi wa hafla hiyo Mama Asha Suleiman Iddi.
Baadhi ya wana jumuiya ya wanafunzi wa Zanzibar wanaosoma chuo Kikuu cha Kiislamu Morogoro wakifuatilia hafla ya maagano kwa wanajumiya wanaotarajiwa kumaliza mafunzo yao mwezi Septemba mwaka huu.
Mwanajumiya ya ZAMUMSA Saleh Haji alitaja baadhi ya changa moto wanazopakabiliana nazo wakati akisoma Risala ya jumiya hiyo katika hafla iliyofanyika kwenye ukumbi wa zamani wa Baraza la Wawakilishi Kikwajuni Mjini Zanzibar.
Mwenyekiti wa ZAMUMSA Bibi Saada akimkabidhi zawadi Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mama Asha Suleiman Iddi kwenye hafla ya kuagana wanajumiiya hiyo wanaomaliza masomo yao mwezi Septemba mwaka huu.
Mama Asha Suleiman Iddi akizungumza na Wana Jumuiya ya ZAMUMSA kwenye ukumbi wa zamani wa Baraza la Wawakilishi uliopo Kikwajuni Mjini Zanzibar.
Mama Asha akimkabidhi Cheti Maalum Mwenyekiti mstaafu wa ZAMUMSA Nd. Rashid Mjaka kwa niaba ya viongozi wenzake baada ya kumaliza muda wao wa utumishi wa jumuiya hiyo. Picha na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ.