Sunday, August 10, 2014

DEREVA TEXI ATOWEKA KATIKA MAZINGIRA YA KUTATANISHA



DEREVA TEXI ATOWEKA KATIKA MAZINGIRA YA KUTATANISHA
Na John Gagarini,Kibaha.

DEREVA wa Texi wa Maili Moja Richard Ponera (36) mkazi wa Mwendapole wilayani Kibaha mkoani Pwani amepotea katika mazingira ya kutatanisha baada ya kukodishwa na watu wasiofahamika.

Ponera alikodishwa na watu wawili ambao hawakufahamika  Agosti 5 mwaka huu majira ya saa 2:30 usiku akiwa anaendesha gari lenye usajili na T 905 BHT aina ya Corolla nyeupe.

Akizungumza na mjini Kibaha kuhusina na tukio hilo katibu wa Umoja wa madereva Texi Kibaha Mjini (KITAGURO) Fadhil Kiroga alisema kuwa dereva huyo tangu alipoondoka siku hiyo hadi leo hakurudi na hakuna taarifa yoyote  iliyopatikana juu yake.

Kiroga alisema kuwa siku ya tukio hilo Ponera alionekana akipatana na watu hao kwa muda kidogo kama dakika 10 hivi kisha akaondoka na watu hao ambao walikuwa wawili.

"Baada ya mapatano licha ya kuwa madereva wengine hawakuweza kujua walichokuwa wakiongea na Ponera waliondoka na alipofika Mlandizi aliwasiliana na mwenzetu ambaye ni Salum Mbawala na kumwambia kuwa kwa sasa yuko Mlandizi," alisema Kiroga.

Alisema kuwa baada ya hapo simu yake haikuweza kupatikana tena kwani baada ya kuona harudi wenzake walijaribu kumpigia lakini simu yake haikupatikana tena.

"Ponera hapa alikuwa hana muda mrefu tangu aanze kazi na alipata gari hilo ambalo alikuwa amekabidhiwa kama wiki mbili zilizopita na gari lenyewe halikuwa kwenye hali nzuri sana kusema labda ilikuwa ni kishawishi cha watu labda kutaka kuliiba gari hilo, hatujui kilichomtokea mwenzetu," alisema Kiroga.

Aidha alisema kuwa wamefanya jitihada mbalimbali ambapo walikwenda polisi kutoa taarifa juu ya tukio hilo na kupewa namba KMM/RB/847/2014 pia walitoa taarifa kwenye vituo vya Mlandizi na Tumbi kisha kutembelea maeneo ya Yombo, Miswe na Mzenga bila ya mafanikio.

Kwa uapande wake mke wa dereva huyo Rosemary Urasa (31) alisema kuwa siku ya tukio hilo alikuja naye hadi Maili Moja yeye akenda sokoni kununua vitu vya nyumbani akamwacha stendi kwa ajili ya kuendelea na shughuli zake kama kawaida.

"Nakumbuka majira ya saa 5 asubuhi nilimpigia simu baada ya gari linguine ambalo liko hapa nyumbani lilikuwa linapiga honi lenyewe nikamwambia aje alizime lakini kwa bahati nzuri kuna mtu alifanikiwa kulizima nikamjulisha alikuwa njiani kuja lakini akarudia eneo linaloitwa Picha ya Ndege, toka hapo kila nikipiga simu simpati," alisema Urasa.

Alibainisha kuwa mumewe ambaye wamezaa naye watoto wawili walihamia Kibaha baada ya kufanikiwa kujenga na kuzaa watoto wawili ambao ni Ruben (14) anayesoma kidato cha kwanza St Anne na Kontrada anayesoma darasa la sita shule ya Msingi Jitegemee.

Aidha alisema kuwa wakati mwingine mumewe hufanya kazi na kukesha hivyo siku hiyo usiku alijua kuwa atakesha lakini ilipofika asubuhi alishangaa kutokumwona kwani endapo anakuwa amekesha asubuhi ni lazima arudi lakini siku hiyo hakumwona ikambidi aje kwenye eneo analopaki lakini alipouliza wakasema tangu alivyoondoka jana hajaonekana tena.

Naye mmiliki wa gari hilo Athuman Kimia alisema kuwa siku hiyo ya tukio aliwasiliana na Ponera ambapo kulikuwa na tatizo la kulipia gari linapokuwa barabarani na kumpa 170,000 kwa ajili ya kulipia.

Kimia alisema kuwa baada ya kama saa moja alimpigia na kumwambia kila kitu kashalipia hivyo mambo mazuri na ndipo alipoendelea na shughuli kama kawaida.

"Tumekubaliana kila baada ya wiki awe ananipa malipo ya kazi lakini nilipigiwa simu kuambiwa kuwa Ponera aonekani na nilipojaribu kumpigia simu yake haipatikani sijui kilichomtokea ninini kwani yeye huwa ananipigia endapo kumetokea tatizo kwani sasa hivi ni wiki ya pili tangu nimkabidhi gari ," alisema Kimia.