KOCHA wa Holland na Manchester United, Louis van Gaal amemwambia mshambuliaji wake supastaa Robin van Persie kwamba atasugua benchi iwapo hatakuwa fiti ipasavyo na pia kama hatacheza kwenye kiwango cha juu.
Van Gaal na nahodha wake Van Persie wanachukuliwa kama watu wenye uswahiba wa aina yake ambao mashabiki wa Manchester United wanautegemea utaisaidia timu pale kocha huyo mkongwe atakapoanza kazi rasmi Old Trafford mara baada ya Kombe la Dunia.
Lakini Van Gaal alimtoa Van Persie dakika 15 kabla ya mchezo kumalizika kwenye mechi ya ushindi wa aina yake dhidi ya Mexico Jumapili usiku ambapo aliyechukua nafasi yake Klaas-Jan Huntelaar alitengeneza bao la kwanza na kufunga la ushindi kwa njia ya penalti.
Klaas-Jan Huntelaar (kushoto) akishangilia bao lake
Alipoulizwa kama Van Persie aliumia, kocha Van Gaal akajibu: "Hapana, mabadiliko ya kumtoa Van Persie yalikuwa ni ya kiufundi.
"Hata hivyo tukumbuke kuwa wakati anajiunga na timu ya taifa alikuwa ametokea kwenye maumivu. Ni vigumu kumchezesha dakika zote 90 hususan katika hali kama hii.
"Kocha anataka ushindi. Hivyo anafanya mabadiliko kadri anavyohitaji. Ni hivyo tu. Hakuna jambo kingine."
Van Perise bado anatarajiwa kuanza kwenye mchezo wa robo fainali Jumamosi dhidi ya Costa Rica lakini kiungo mkabaji Nigel de Jong hatarajiwi kuwa fiti kufuatia maumivu ya nyonga yaliyomlazimisha kutolewa mapema kwenye mechi ya Mexico.