Na Mwandishi Maalum, New York
Baada ya vuta ni kuvute ya muda mrefu na majadiliano makali baina ya nchi zinazotoa walinzi wa Amani ( TCC) na zile zinazochangia raslimali fedha, hatimaye siku ya alhamisi ( Julai 3, 2014) Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, lilipitisha nyongeza ya posho kwa walinzi wa amani kutoka posho ya sasa ya dola za kimarekani 1, 028 kwa mwezi hadi dola za kimarekani 1,410 kwa mwezi.
Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, lilipitisha nyongeza hiyo baada ya Kamati ya Tano inayohusika na masuala ya Utawala na Bajeti kukamilisha majadiliano ambayo yamedumu kwa miezi miwili na wakati mwingine yaliendelea usiku kucha ili kufikia makubaliano ya nyongeza hiyo ambayo haijawahi kufanyiwa marekebisho kwa zaidi ya miaka 20.
Kwa mujibu ya makubaliano yaliyofikiwa kati ya pande hizo mbili yaani nchi zinazotoa walinzi wa Amani ambao wengi wao wanatoka nchi za Asia ya Kusini na Afrika na wachangiaji wakubwa wa raslimali fedha wakiwamo Japani , nyongeza hiyo ya posho kwa walinzi wa Amani itakuwa ikiongezeka kwa awamu tatu.
Mgawanyo huo itakuwa kama ifuatavyo, Julai mosi 2014 nyongeza ya posho itakuwa dola za kimarekani 1,332. Julai Mosi 2016 itaongezeka na kuwa dola za kimarekani 1,365 na awamu ya tatu itaanza Julai Mosi 2017 ambapo posho itakuwa dola za kimarekani 1,410 kwa mwezi .
Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, litapitia nyongeza hiyo ya posho baada ya miaka minne. Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kupitia Uwakilishi wake wa Kudumu katika Umoja wa Mataifa, umeshiriki kikamilifu katika mchakato mzima wa majadiliano hayo ambayo hatimaye yaliwezesha kufikia muafaka wa nyongeza hiyo.
Nyongeza hiyo posho ya dola za kimarekani 1,410 kwa mwezi ni tofauti na pendekezo lililotolewa na Jopo la wataalamu waliopewa jukumu ya kufanya utafiti wa kisayansi ili kupata kiwango stahili cha nyongeza ya posho hasa kwa kuzingatia gharama kubwa ambazo nchi zinazotoa wanajeshi na vifaa zilikuwa zikitumia katika maandalizi, lakini pia mazingira magumu na hatarishi ambayo walinzi hao wa Amani wanakabiliana nayo.
Baada ya utafiti huo Jopo hilo la Wataalamu lilikuja na pendekezo la nyongeza ya dola za kimarekani 1,762 kwa mwezi wa kila mlinzi wa Amani anayehudumu katika ulinzi wa Amani katika Umoja wa Mataifa. Ingawa pendekezo hilo la dola 1,762 liliungwa mkono na nchi zinazotoa wanajeshi wao, lakini ilikuwa gumu kukubaliwa na nchi zinazotoa raslimali fedha licha ya kwamba kama ilivyokuwa kwa watoa walinzi wa Amani, nazo zililidhia kufanyika kwa utafiti huo wa kisayansi .
Pamoja na kupitisha nyongeza hiyo ya posho kwa walinzi wa Amani, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa pia limepitisha Bajeti ya Operesheni za Ulinzi wa Amani ambayo imefikia dola za kimarekani 7 bilioni kwa mwaka. Aidha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa katika kikao chake cha Alhamisi pia kimepisha dola za kimarekani 7.5 milioni kwaajili ya mzunguko wa vifaa na zana za kijeshi.
Kupitishwa kwa fedha hizo kumetokana na pendekezo lililotolewa na Kikundi Kazi kuhusu vifaa na zana za kijeshi ambazo hutolewa na nchi zinazotoa walinzi wa Amani. Dola hizo 7.5 milioni ni sehemu ya bajeti ya jumla ya Operesheni za kulinda Amani yaani dola za kimarekani 7 Bilioni. Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kati ya nchi zinazoongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya walinzi wa Amani wanaohudumu katika Operesheni za Kulinda Amani za Umoja wa Mataifa.
Sehemu ya Walinzi wa Amani wa MONUSCO katika Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wakiwa katika moja ya utekelezaji wa dhamana ya kulinda amani. Julai 3 Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limepitisha nyongeza ya posho kwa walinzi wa amani kutoka dola za kimarekani 1,028 kwa mwezi hadi dola za kimarekani 1,410 kwa mwezi badala ya 1,762 kiwango kilichokuwa kimependekezwa na Jopo la Wataalam baada ya utafiti wa kina.