Sunday, July 27, 2014

MPIGANAJI HENRY LYIMO (KIPESE) WA MOSHI AFARIKI DUNIA KATIKA AJALI YA PIKIPIKI


MPIGANAJI HENRY LYIMO (KIPESE) WA MOSHI AFARIKI DUNIA KATIKA AJALI YA PIKIPIKI
Marehemu Henry Lymo maarufu kama Kipese.
Na Dixson Busagaga
TASNIA ya Habari na michezo mkoani Kilimanjaro imepata pigo kufuatia kifo cha ghafla cha Mtangazaji wa kituo cha radio cha Moshi FM Henry Lyimo, maarufu kama Kipese. Marehemu Kipese amefariki dunia usiku wa jana akiwa njiani akitokea Rombo katika eneo la njia Panda, Himo,  baada ya pikipiki aliyokuwa akitumia kugongana na pikipiki nyingine. 

Taarifa za awali zinasema Marehemu Kipese alikuwa akitokea wilayani Rombo ambako amekuwa akifanya shughuli zake na kwamba wakati anarejea ndipo mauti yakamfika baada ya kuumia vibaya katika ajali hiyo.

Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika hospitali ya Kilema wilayani Rombo kungojea taratibu nyingine toka kwa ndugu zake.
Tayari makundi mbalimbali ambayo marehemu amekuwa karibu nayo kwa shughuli za kikazi yametoa taarifa za masikitiko kufuatia kifo cha Kipese huku yakipanga kukutana asubuhi hii kwa ajili ya kupanga mambo mbalimbali kwa ajili ya kufanikisha mazishi hayo.

Kundi la kwanza ni kundi la waandishi wa habari mkoa wa Kilimanjaro kupitia klabu yake ya Media Club of Kilimanjaro wamepanga kukutana asubuhi hii katika eneo la Posta. Kundi la pili ni la wafanyakazi wote wa Moshi FM radio ambako marehemu alikuwa akifanya kazi hadi Mauti yanamkuta wamepanga kukutana asubuhi hii kuanzia majira ya saa 2.

Kundi la tatu ni la wadau wa michezo mkoani Kilimanjaro ambako licha ya kwamba Marehemu Kipese alikuwa mtangazaji wa kipindi cha Michezo katika radaio aliyokuwa akifanyia kazi pia alikuwa mwamuzi wa mchezo wa soka. Wadau hao wamepanga kukutana katika ofisi za chama cha soka mkoa wa Kilimanjaro (KRFA) kujadili namna ya kushiriki msiba huo mzito kwa tasnia ya habari na michezo.
Globu ya Jamii inaungana na famili, ndugu jamaa na marafiki wa marehemu katika kuomboleza msiba huu mzito. 

Matokeo ya Utafutaji

  1.  Inna Lillahi Wa Inna Ilahi Raaji'oon