Sunday, February 26, 2017

Rais Magufuli Atoa Mkwala Mzito Kwa Wanaojenga Bomba la Mafuta Kutoka Tanga Hadi Uganda..


Rais Magufuli Atoa Mkwala Mzito Kwa Wanaojenga Bomba la Mafuta Kutoka Tanga Hadi Uganda..
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr.John Pombe Magufuli amesema hatavumilia uzembe wa aina yoyote katika ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Tanga hadi Hoima nchini Uganda bali anataka ujenzi wa bomba hilo ufanywe katika hali inayotarajiwa ili wananchi wa Uganda na Tanzania wanufaike nalo.

Dr.Magufuli ametoa onyo hilo Ikulu jijini Dar es salaam  mara baada ya kushuhudia utiaji saini wa mkataba wa ushirikiano baina ya Tanzania na Uganda uliofanyika mbele yake na Rais wa Uganda Yoweri Kaguta museveni ambaye yupo nchini kwa ziara ya kikazi ya siku mbili.

Aidha Rais DKt.magufuli amemweleza mgeni wake Rais Museveni kuwa Tanzania imeanza kujenga reli kutoka Dar es Salaam hadi mkoani Mwanza kwa kiwango cha kisasa yaani Standard Gauge ambapo itakapofika mkoani Mwanza atajenga bandari kavu maalum kwa ajili ya kuhudumia wafanyabiashara wa Uganda pekee.

Naye Rais Museveni amesema nchi ya Uganda inaitambua Tanzania kama rafiki wa kweli na kwamba atashirikiana na Rais Dr.Magufuli katika nyanja zote lengo kuu likiwa ni kuwafanya watanzania na waganda waweze kuishi maisha bora zaidi ya hivi sasa.

Baadhi ya nyanja ambazo Tanzania na Uganda wamekubaliana ni kuimarisha biashara miongoni mwao,kushirikiana katika usafiri wa anga,mawaziri wa mambo ya nje kukutana mara kwa mara na kujadiliana jinsi ya kuboresha uhusiano baina ya mataifa.