Tuesday, September 11, 2012

WANAHABARI WAMTIMUA WAZIRI NCHIMBI KATIKA MAANDAMANO YAO.


 


Katibu wa Jukwaa la Wahariri Bw. Nevil Meena akiongea kwa uchungu mbele ya wanahabari wenzake ambapo pamoja na maazimio mengine wametangaza kutoandika habari zinazohusiana na jeshi la polisi kwa siku 40. 






Na Datus Boniface.
Wakiwa katika nyuso za huzuni kubwa ya kuondokewa na mwenzao ambaye aliuawa kwa kupigwa na bomu, kundi la Wanahabari wao wamemtimua Waziri wa Mambo ya Ndani Mh. Emmanuel Nchimbi kutokana na kuwaingilia kwenye maandamano yao.
Wanahabari kote nchini leo wamefanya maandamano ya amani kwa lengo la Kulaani mauaji ya mwenzao wa kituo cha Televisheni cha Channel Ten, Daudi Mwangosi.
Kufukuzwa na kuzomewa kwa Waziri Nchimbi kumekuja baada ya kugundulika kuwa ameingilia maandamano kwa lengo la kuyapokea bila kupewa mwaliko.
Kutokana na zomea zomea hiyo ya wanahabari hao dhidi ya Waziri Nchimbi hali ilionekana kuwa si shwari na kupelekea waziri huyo kuondolewa na rais wa UTPC Keneth Simbaya na viongozi wengine wakiwemo askari polisi.
Akizungumza na kundi la waandishi Katibu wa Jukwaa la Jukwaa la wahariri (TEF) Neville Meena amesema “Hatuna ugomvi na Waziri Nchimbi kwani ni mwenzetu, rafiki yetu, ila leo hana vazi la msiba”
Mara baada ya kuondoka bila kupenda Waziri Nchimbi, hali ya utulivu ilikuwa kama kawaida na shughuli zingine ziliendelea kama ilivyopangwa.