Sisi Maaskofu, Mapadre, Wachungaji na Waumini tunaoishi Zanzibar, tumekutana leo tarehe 30 Mei 2012 kufutia hali ya machafuko, uvunjifu wa amani, uchomaji wa Makanisa, uharibifu wa mali za Kanisa na vitisho dhidi ya Wakristo na mali zao.
Tumekutana na tunatoa tamko baada ya muda mrefu wa kimya na uvumilivu tuliosafiri nao kwa takribani miaka 11, kwa kumbukumbu zetu tangu mwaka 2001. Tunajua na tunauambia umma wa wapenda amani kuwa matukio ya tarehe 26 hadi 28 Mei 2012 ni matokeo ya mahubiri na mihadhara
ambayo imekuwa ikiendeshwa iliyolenga kwa makusudi kuutukana na kuukashifu Ukristo hapa visiwani Zanzibar na hivi kupandikiza hofu miongoni mwa waumini wa dini ya Kikristo. Tunashawishika kusema kuwa ufadhili na ushawishi wa vurugu na vitisho hivi vina udhamini wa ndani au nje ya nchi yetu.
Tumefikia hatua hiyo baada ya matukio mbalimbali yaliyokuwa yanafanywa dhidi ya Kanisa na mali zake tangu mwaka 2001 hadi hivi majuzi yalikuwa yakitolewa taarifa kwenye vyombo vya Ulinzi na Usalama hapa visiwani Zanzibar lakini ushirikiano umekuwa mdogo na kwa sehemu kubwa
dhaifu sana. Kwa maelezo na vielelezo ni kwamba, jumla ya makanisa yasiyopungua 25 yamevunjwa na kuchomwa moto tangu mwaka 2001, pamoja na ahadi za Serikali na vyombo vya ulinzi na usalama katika maeneo yote yaliyopata kutolewa taarifa hakuna hata moja lililothibitikawahusika kukamatwa, kufikishwa mahakamani na kuchukuliwa hatua za kisheria. Kumekuwa pia na vitendo vya kuchoma magari huko Pemba na hapa Unguja, na Serikali kwa upande wake imeshiriki hata kupora ardhi na majengo ya Kanisa hapa Unguja na huko Pemba.
Tumebaini pia hasa baada ya matukio ya vurugu za tarehe 26 hadi 28 Mei 2012 kuwa kuna mikakati ya makusudi ya kuwafanyia Wakristo vurugu. Mikakati hiyo inajumuisha mambo kama vile kuchoma Makanisa zaidi, kuharibu mali za Makanisa yakiwemo mashule, vituo mbalimbali vya Kanisa vinavyotoa huduma za kijamii hapa Visiwani.
Mkakati au mpango huo umepangwa na unakusudiwa kutekelezwa kati ya tarehe 1 na 2 Juni, na tarehe 8 na 9 Juni mwaka huu. Tunazo taarifa tunazoweza kuzithibitisha kuwa baadhi ya Wakristo wamekuwa wakitumiwa jumbe za simu za mkononi (SMS) zikiwatisha na kuwataka waondoke visiwani humu mara moja hata kama ni wazawa.
Sehemu ya pili ya mkakati ni kuwasaka Wakristo nyumba kwa nyumba kwa ajili ya kuwaangamiza, kuwabaka na kuwalawiti.
Chakusikitisha zaidi ni pale ambapo baadhi ya walinzi wa Usalama wa raia hasa Polisi wenye asili ya hapa Visiwani Zanzibar kusikika wakisema kuwa wataunga mkono vurugu kila zitakapotokea.
Kufuatia maelezo hayo yote, Sisi Maaskofu, Wachungaji, Mapadre na waumini tuliokutana leo, tunapenda kwanza kutoa neno la shukrani kwa uongozi wa Serikali kwa ushirikiano iliyotuonyesha kufutia matukio ya hivi majuzi, na hasa kwa kupewa fursa za kukutana na viongozi na kusikilizwa.
Tunatamka kuuelezea umma wa wapenda Amani wote tukisema, tumechoswa kuishi na kuchukuliwa kama raia wa daraja la pili katika nchi yetu. Tunaonya kuwa hatuko tayari tena kuvumilia vitendo vya uvunjaji wa amani na haki zetu na tabia za kufanywa tuishi kwa hofu.
Kadhalika tunaiomba seriakli yetu ituhakikishie usalama wa maisha yetu, mali zetu pamoja na majengo yetu ya ibada.
Wito wetu kwa viongozi wa dini mbalimbali hapa nchini ni kuwa, kila mmoja anawajibu mkubwa wa kuhakikisha kwamba nchi yetu inatawaliwa kwa mujibu wa sheria za nchi na kwmba kila mmoja ahubiri kwa lengo la kukuza amani, utulivu na usalama wa kila mtu na mali zake.
Mwisho, tunapenda kuhitimisha tamko letu kwa kuwaalika wakristo wote kuiombea nchi yetu amani, utulivu na mshikamano ambazo ni tunu tulizoachiwa na waasisi wetu.
Ni imani yetu pia kwamba viongozi wetu wataendeleza wajibu wao na mamlaka waliyopewa na Mungu pasipo upendeleo wa aina yoyote.
Mungu Ibariki Tanzania, Mungu Ibariki Zanzibar.
Kwa niaba ya Wakristo wote;
Ni sisi Maaskofu wenu
1. Michael Hafidh
Askofu wa Kanisa Anglikana Zanzibar
2. Augustine Shao
Askofu wa Jimbo Katoliki Zanzibar
3. Pastor Timothy W. Philemon
Makamu Mwenyekiti wa Ushirika wa Wachungaji wa Makanisa ya Pentekoste Zanzibar
SOURCE: Kiongozi Toleo Na: 22 Juni 01-07,2012 (uk 2).