Friday, June 01, 2012

Uzinduzi wa Taarifa ya Haki za Binadamu

Ripoti ya Haki za Binadamu Tanzania ni ripoti ambayo imekuwa ya msaada mkubwa sana katika kulinda na kutetea haki za binadamu nchini. Ripoti hii pia imekuwa  chachu ya mabadiliko katika sera na sheria mbali mbali katika mfumo wa utawala wetu. Na zaidi imekuwa nyenzo ya kufundishia haki za binadamu katika maeneo mbali mbali kama vile vyuo vikuu, shule za sekondari, wasaidizi wa sheria na waangalizi wa haki za binadamu.

 

Ripoti hii ya haki za binadamu inagusa maeneo yote ya haki za binadamu. Maeneo ambayo yamefuatiliwa zaidi ni pamoja na haki za kisiasa na kiraia,haki za kiuchumi, kijamii na kiutamaduni; haki za makundi maalum; vyombo vinavyohusika na ulinzi pamoja na utetezi wa haki za binadamu; masuala ya utawala bora na rushwa. Inaeleza ni kwa namna gani Tanzania kama taifa inavyoheshimu na kulinda haki za binadamu kwa kufuata mikataba ya haki za binadamu ya kimataifa.

 

Ripoti hii pia inaeleza kwa kina ukiukwaji wa haki za binadamu. Wataalam wetu watatueleza kwa kifupi nini kimeandikwa katika kila sura. Ripoti imebaini ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu unaofanywa na vyombo vya dola hususani polisi; pia mauaji ya vikongwe kwa imani za kishirikina, ukatili wa kijinsia na watoto; mimba za utotoni; kuporomoka kwa ubora wa elimu nchini, wabunge wasio hudhuria vikao vya Bunge na wanao lala bungeni, huduma duni za afya, huduma duni za makazi ya askari wetu; na kukosekana kwa motisha ya kufanya kazi kwa askari na watalaam katika sekta ya habari. Lakini pia ni vyema pia nikazungumzia suala la ukwepaji kodi katika nchi kama ilivyotazamwa katika sura ya tisa ya ripoti hii.

 

Nchi yeyote duniani ili iweze kuendelea inahitaji kodi. Kodi ni uhai wa uchumi wa nchi ili iweze kuwaletea maendeleo wananchi wake. Ripoti imebaini kuna makampuni mengi ambayo yanakwepa kulipa kodi ama yanalipa kidogo sana kuliko kile ambacho wangestahili kulipa. Katika bunge la bajeti 2011/12 Mh. Waziri mkuu alitaja orodha ya walipa kodi bora 15 nchini. Ni ukweli usiopingika kuwa kwenye orodha ile kuna makampuni makubwa ya mawasiliano, makampuni makubwa ya vinywaji, makampuni makubwa ya uchimbaji madini, makampuni makubwa ya udhalishaji bidhaa za chakula na mengine mengi ambayo yangekuwa yanalipa kodi yangeweza kuwepo kwenye nafasi za juu lakini haikuwa hivyo.

 

Mwalimu Nyerere katika hotuba yake ya siku ya wafanyakazi kule Mbeya mwaka 1995 aliihimiza serikali kukusanya kodi. Mwalimu aliamini kodi ndio nguzo pekee ya kuweza kukuza uchumi wa ndani wa nchi. Lakini leo inastaajabisha sana kuona kodi inalipwa na kundi dogo la watanzania hususani wafanyakazi walioajiriwa katika sekta rasmi. Makampuni makubwa hayalipi kodi, wafanyabiashara hawalipi kodi, wananchi katika sekta isiyo rasmi hawalipi kodi hivyo basi ipo haja kwa serikali kuongeza wigo wa walipa kodi ili kunusuru uchumi wa nchi.

 

Tunaomba vyombo vinavyohusika na ukusanyaji kodi kuwajibika kwa uzalendo wa kweli kwa nchi. Mamlaka ya mapato pamoja na halmashauri za wilaya ziwajibike kwa manufaa ya watanzania na si kwa maslahi binafsi. Elimu ya mlipa kodi itolewe kwa watanzania ili kuelewa umuhimu wa kulipa kodi kwa maendeleo ya uchumi. Tukiweza kukusanya mapato yetu ya ndani kwa kiwango cha juu uchumi wetu utaimarika na hivyo kumkomboa mtanzania kutoka katika wimbi la umaskini.

 

Mwisho natoa shukrani tena kwa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kwa kuweza kutoa ripoti ya hali ya Haki za Binadamu kila mwaka. Hiki ni kipimo kizuri kwa uwajibikaji, kulinda na kutetea haki za binadamu nchini. Nitoe rai yangu kwa yeyote aliyetajwa katika ripoti hii, iwe ni mtu binafsi au taasisi kujisahihisha ili kuleta mabadiliko ya kweli.

 

Uzinduzi wenyewe ni kama ifuatavyo:

 

Tulikotoka, tuliko na tunakoelekea:

                   2002, taarifa ya Kwanza                                                              2006: Taarifa ya Mwisho kwa Tz Bara pekee                            Taarifa ya Kwanza; ikijumuisha na Zanzibar

 

Watafiti cum  Waandishi

 

 

                                          ole Ngurumwa                                                                           Bw. Mlowe                                                             Bi. Harous Mpatani

 

 

 

Wageni Rasmi

 

                                                Balozi wa Sweden                                                                                                    Prof. Lipumba                 

 

 

                                                          Ukataji wa Ribon

 

 

                                                                                          Makofi kwa Uzinduzi

 

 

                                                                   Taarifa Oyee!

 

 

 

 

Wadau wa Maendeleo