Sunday, April 05, 2015

WAFIPA WANAVYOTUMIA RADI KUTUMA SALAM



WAFIPA WANAVYOTUMIA RADI KUTUMA SALAM



WAFIPA ni miongoni mwa makabila ya Kibantu na linalopatikana katika mkoa wa Rukwa na mkoa wa jirani wa Katavi.


Ingawa Wafipa wametawanyika sehemu mbalimbali nchini makao makuu ya kabila hilo ni Sumbawanga na ndio kabila kubwa zaidi katika mkoa wa Rukwa. Kama ilivyo kwa makabila mengine ya kibantu Wafipa wana mila na desturi zao. Ingawa Wabantu wana mfumo wa kufanana kama ilivyo kwa makabila mengine, Wafipa wana mila na desturi zinazowatofautisha na makabila mengine nchini.

Wafipa ni miongoni mwa makabila yanayodhaniwa kuwa na uchawi na uwezo mkubwa wa kutumia sayansi kutengeneza zana za kijadi kwa ajili ya mawasiliano, ulinzi na usafiri. Katibu Mtendaji wa Chama cha Mila na Desturi za Kabila la Wafipa (Midekawa) mkoani Rukwa , Domislau Mtuka, anasema mfumo wa awali wa maisha ya Mfipa ulisababisha wageni kujenga dhana kuwa kabila hilo linatumia uchawi.
Mtuka ambaye anatoka katika ukoo wa kichifu wa kabila la Wafipa anasema uadilifu uliotukuka na hali ya kujiamini ndio iliyosababisha watu kudhani kuwa Wafipa ni wachawi jambo ambalo sio kweli.
"Zamani hapakuwepo na Mfipa mwizi, mvivu wala anayefanya maovu hivyo waliacha mali hasa mifugo bila walinzi na kwenda kwenye shughuli za uzalishaji au za kijamii jambo lililosababisha makabila mengine kudhani kuwa mali hizo zinalindwa kwa kutumia uchawi," anaeleza Mtuka.
Uadilifu uliwajengea Wafipa imani kuwa hakuna atakayeweza kuiba mifugo hivyo walikuwa wanaachia ng'ombe kwenda malishoni na kurudi wenyewe. Wageni walipoona ng'ombe wanakwenda malishoni na kurejea wenyewe walistaajabu na ndipo walipojenga dhana kuwa uchawi unatumia kuwaswaga ng'ombe kwenda malishoni.
"Wageni hawakuzingatia hali halisi kuwa ng'ombe wana uwezo wa kukumbuka njia ya kurudi kwenye zizi bila kuelekezwa, wao walieneza uvumi kuwa uchawi unatumika na uvumi huo uliendelea kuwepo kupitia simulizi," anasema Mtuka. Mtuka anaeleza kuwa uvumi kuwa Wafipa ni wachawi ulienea kwa kasi baada ya wageni kupigwa radi na kuunguzwa au kuuawa kila walipojaribu kuiba mifugo na mazao ya Wafipa.
Wageni hao waliadhibiwa baada ya mwenye mali kutoa taarifa kwa wazee wa jadi ambao waliamuru kupigwa mbiu kwa siku tatu mfululizo ili wahalifu warejeshe mali waliyoiba. Mbiu ilipigwa pia katika vijiji jirani ili taarifa ziweze kuwafikia wote waliohusika kwenye wizi huo.
Mtu aliyepatikana na hatia alipewa adhabu ya kuunguzwa nywele kwa kutumia radi ambapo nywele zilibaki majivu bila kupata jeraha lolote mwili au pia kuunguza nguo yake ya ndani na kuwa majivu bila kumdhuru sehemu zake za siri . Mtuka anasema radi ya Wafipa ilitengenezwa kwa kutumia utaalamu maalum na sio radi inayosababishwa na miale mikali ya umeme inayosababishwa na mingurumo wakati wa mvua.
Anafafanua kuwa radi ya kienyeji ilitengenezwa na wazee wenye utaalamu muhimu ambao hivi sasa wamebaki wachache kutokana na mabadiliko ya mfumo wa maisha ambapo hivi sasa Wafipa wameacha mila na desturi na kazi ya ulinzi na usalama inafanywa na polisi.
Kwa mujibu wa Mtuka, mtambo wa kutengenea radi ulibuniwa na kutengenezwa na wavumbuzi wa sayansi ya asili enzi hizo ilitumika kama sihala ya kujihami dhidi ya maadui kabla kabila hilo la wafipa hawajaanza kubuni na kutengeneza bunduki za kienyeji maarufu kama 'magobole' .
Anadai kuwa radi hiyo pia ilitumika pia kulinda himaya ya mtemi dhidi ya maadui wake . Pia radi hiyo ilitumika kama njia ya mawasiliano kati ya mtemi na mtemi hasa wakati wa kusalimiana na kutumiana ujumbe maalum. Pia radi ilitumiwa kutuma salamu kati ya marafiki waliyoshibana ambapo radi ikitua kwa mhusika iliacha ishara bila kusababisha madhara yeyote.
"Inaelezwa kuwa radi iliweza kwenda masafa marefu na kutua eneo lililolengwa na kuacha ishara ambao mwenye eneo alikuwa na uwezo wa kuitafsiri na kujibu kwa kutumia radi au kusafiri hadi kwa mtuma radi ili kufanya mkutano. "Hivyo mtu akirudi nyumbani kwake na kukuta ishara iliyoachwa na radi alibaini kuwa fulani alikuwa anamsalimia hivyo naye alimtumia radi kumjulisha kuwa salamu zimefika " alieleza .
Anakiri kuwa enzi hizo watu wengi wa kabila hilo la Wafipa walikuwa wakimiliki mtambo wa kutengeneza radi kuliko ilivyo sasa ambapo hawako radhi kujionesha hadharani na kutoa huduma hiyo kwa wateja wao kwa usiri kubwa . Anaeleza kuwa asili ya radi hiyo inayotengezwa kienyeji ilibuniwa na kutengenezwa na wazee wa jadi hasa walinzi wa Mtemi ambao walitumia teknolojia ya asili kutengeneza zana mbalimbali.
"Simulizi za historia ya Wafipa zinasema kuwa wavumbuzi hao wa sayansi ya asili walikuwa na vipaji na wabunifu hivyo wali walifanikiwa kuvumbua mambo mengi ukiwemo mtambo wa kutengenezea radi ambayo ikitengwa na kuamuriwa kupiga hata mchana kweupe bila kuwepo na mvua, " anasema.
Anavitaja baadhi ya vifaa muhimu ambavyo vinatumika kutengezea mtambo huo wa radi kuwa ni pamoja na njugu nyekundu , sindano mpya ambayo haijatumika kabisa na kipande cha nyoka aitwae tia ambaye anauawa kwa dawa za asili. Ilidaiwa kuwa ikuwa mwiko kutumia nyoka aliyeuawa kwa kutumia zana za kisasa ikiwano bunduki kwa sababu radi hiyo haitalipuka.
Pia ilikuwa mwiko kumwambia mke kuhusu utengenezaji wa radi, iwapo mke anafahamu siri ya mume kuhusu kutengeneza radi basi ni udhibitisho kuwa wote wanashirikiana.
"Utaalamu huo wa kumiliki mtambo wa radi na usafiri wa kutumia ungo maarufu kama 'ndege ya juu' haurithishwi kwa watoto hovyo hovyo bali kwa kuzingatia karama na kipaji cha mtoto husika. Urithi huo hutolewa kwa kuzingatia mambo ya kimila pasipo ubaguzi wa kijinsia na mtoto anaweza kuwa wa kike au wa kiume na hurithishwa kwa siri akiwa bado mchanga bila hata mama yake kujua.
Wakati wa kurithishwa utaalamu huo mtoto anawekewa kiganjani kifaa maalumu kinachotumika kutengenezea mtambo huo. Endapo mtoto ataweza kukunja kiganja chake na kushika kifaa hicho ni dalili kuwa amekubali na atakuwa mtiifu maisha yake yote pia kuitunza siri hiyo.
Kama mtoto atashindwa kukunja viganja vya mkono na kuacha kifaa kidondoke ni ishara kuwa amekitupa na hivyo hawezi kurithi. Pia Wafipa walikuwa na mfumo wa kusikiliza kesi na kutoa adhabu ya kulipa faini endapo mtuhumiwa atakutwa na hatia. Ingawa utaratibu huo hautumiki sana siku hizi bado wapo Wafipa wachache wanaoutumia na endapo mtu atapatikana na hatia analipa kati ya Sh 2,000 hadi 20,000 kulingana na ukubwa na uzito wa tatizo lenyewe .
Wavumbuzi wa sayansi ya asili waliweza kuvumbua namna ya kutengeneza moto na kuuhifadhi kwa kutumia miti ya asili kwa zaidi ya saa 48 bila kuzimika. Hata hivyo hazina ya miti hiyo kwa sasa imeshatoweka kutokana ukataji na uchomaji moto ovyo wa misitu ya asili.