Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Mh. Injiania Binilith Mahenge awapa miezi sita kiwanda cha East coast oil and edible kinachozalisha vipodozi na mafuta ya kupikia kilichopo Kurasini jijini Dar es Salaam kusimamisha uzalishaji wake unaoendeshwa kwa kutumia nishati ya magogo .
Akiwa katika mwendelezo wa ziara zake za ukaguzi mazingira Mh. Mahenge alimtaka Mkurugenzi mtendaji wa kiwanda hicho Bwana Vijay Raghavan kutumia nishati mbadala kama gesi katika uendeshaji wa mitambo ya uzalishaji wake.
Katika ziara hiyo Mh. Mahenge alibaini kuwa tani 50 za magogo huteketezwa kila siku kiwandani hapo kwa ajili ya uendeshaji wa mashine za uzalishaji jambo ambalo huhatarisha mazingira ikiwemo Mabadiliko Tabianchi.
Hata hivyo alikitaka kiwanda hicho kuboresha mfumo wake wa maji taka yanayotiririshwa kuelekea baharini kwa kuyatibu ili kuondoa sumu inayowaathiri viumbe hai washio baharini pamoja na watu wanaotumia samaki hao kama vitoweo.
Wakati huo huo Mh. Mahenge alitembelea pia fukwe za Mbezi mtaa wa Malecela kuitikia wito wa malalamiko ya wananchi khusu uvamizi wa eneo la Ufukwe huo, ambapo alithibitisha kuwepo kwa uvamizi wa eneo hilo.
Akizungumza na mwenyekiti wa mtaa huo Bwana SIlas Malipula Mh. Mahenge alisema kuwa uendeshaji wa shughuli za maendeleo uliofanyika na unaoendelea ndani ya mita 60 kutoka eneo la hifadhi ya mikoko ni kosa kisheria hivyo Wizara yake imelipokea na italifanyia kazi .
Mheshimiwa Mahenge aliongeza kuwa swala la utunzaji wa Mazingira ni letu sote hivyo kila Mwananchi anatakiwa kuwa makini ili kuzuia uharibifu unaoendelea katika maeneo mbalimbali nchini
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais -Mazingira Injinia Binilith Satano Mahenge (wa tatu kushoto) akitoa Maagizo ya kusitisha kwa matumizi ya magogo katika Kiwanda cha East Coast Oils and Fats, ambapo magogo hayo huyatumia katika shughuli za uzalishaji wa bidhaa mbalimbali kiwandani hapo.Kulia kwake ni Mkurugenzi Mtendaji Bw. Vijay Raghavan.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais -Mazingira Injinia Binilith Satano Mahenge (aliyetangulia) akitembelea Kiwanda cha East Coast Oils and Fats kilichopo Kurasini jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais- Mazingira Injinia Binilith Satano Mahenge (katikati) akionyeshwa ramani ya sehemu ambayo mikoko imekatwa na Baadhi ya wananchi ili kupisha Ujenzi ambao si halali katika fukwe za Bahari ya Hindi eneo la Mbezi Beach Jijini Dar es Salaam. Anayemwonyesha ni Mwenyekiti wa Mtaa wa Malechela Silas Malipula.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira Injinia Binilith Satano Mahenge (katikati) akionyesha Bango linalokataza Ujenzi wa pembezoni mwa ufukwe likiwa limeondolewa na mmoja wa wamiliki wa nyumba za Ufukweni ili kupisha ujenzi wa nyumba yake uendelee.