Thursday, January 15, 2015

JESHI LA POLISI LAZIDI KUWATIA MBARONI PANYA ROAD, SASA IDADI YAFIKIA 1508


JESHI LA POLISI LAZIDI KUWATIA MBARONI PANYA ROAD, SASA IDADI YAFIKIA 1508
Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linaendelea na msako mkali wa kuwakamata na kuwadhibiti vijana wanaofanya uhalifu wa makundi maarufu kwa jina la Panya Road. 

Msako huo mkali ni endelevu kama ilivyokwishaelezwa tangu awali mpaka tutakapohakikisha uhalifu wa makundi au jina la panya road litakapofutika kabisa. Misako hii inafanyika katika mikoa yote ya kipolisi yaani Ilala, Temeke na Kinondoni na makamanda wa mikoa hiyo wanaendelea kuwa wasimamizi wakuu wa misako hii.

Misako hii iliyoanza tarehe 03/01/2015 hadi sasa imefanikisha kuwakamata vijana wapatao 1508 wakituhumiwa kwa makosa mbalimbali yakiwemo ya kujeruhi,wizi, dawa za kulevya, kupatikana na bhangi, wapiga debe na kubugudhi abiria, kucheza kamari, biashara ya ukahaba, mirungi, mikusanyiko isiyo halali katika vijiwe n.k. Uzoefu unaonyesha kwamba maeneo na vitendo tajwa hapo juu huchochea vijana kufanya uhalifu wa aina mbalimbali ambao pia ni kero kwa wananchi.

Pamoja na watuhumiwa hawa wote  kukamatwa, hadi sasa watuhumiwa wapatao 959 tayari wamefikishwa katika mahakama mbalimbali jijini Dar es Salaam kwa tuhuma zilizotajwa hapo juu. Mashauri yao yanaendelea katika mahakama hizo kwa hatua mbalimbali za kutajwa, kusikilizwa, n.k.

Aidha, watuhumiwa wapatao 430 wameachiwa kwa dhamana kusubiri kukamilisha upelelezi huku nyendo zao zikifuatiliwa kwa kushirikiana na wazazi wao na viongozi katika maeneo yao. Watuhumiwa 119 wameachiwa huru baada ya kukosekana kwa ushahidi wa kutosha lakini pia nyendo zao zinafuatiliwa na endapo watabainika wanajihusisha na uhalifu basi watakumbwa na msako unaoendelea.

Natoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa za uhakika kama wanavyofanya hivi sasa ili makundi yanayofanya uhalifu wa aina ya panya road yatokomezwe kabisa ikiwa ni pamoja na uhalifu mwingine wa aina yoyote. Nataka wananchi wa jiji la Dar es Salaam na watanzania kwa ujumla waishi na kufanya shughuli zao za kijamii na kiuchumi kwa amani na utulivu uliozoeleka.

S.H. KOVA,
KAMISHNA WA POLISI KANDA MAALUM,
DAR ES SALAAM.