Monday, April 25, 2016

SERIKALI YAOMBWA KUTENGA FEDHA KILA MWAKA KWA AJILI YA UKARABATI WA SHULE KONGWE YA ILBORU



SERIKALI YAOMBWA KUTENGA FEDHA KILA MWAKA KWA AJILI YA UKARABATI WA SHULE KONGWE YA ILBORU
Na Woinde Shizza,Arusha.
SERIKALI imeombwa kuendelea kutenga fedha za ukarabati kila mwaka kwa shule kongwe ya wanafunzi wenye vipaji maalum ya Ilboru ili walau kuzirudisha katika hali yake nzuri na kuzijengea mazingira mazuri ya kujifunzia na kufundishia, ili zionekane tofauti na shule zingine hatimaye ziwafanye wanafunzi wajitume zaidi katika masomo.

Hayo yalisemwa jana na mkuu wa shule kongwe ya Ilboru sekondari Julius
Shulla alipokuwa akizungumza na wadau wa elimu na walezi katika mahafali ya 24 ya kidato cha sita yaliyofanyika shuleni hapo.

Alisema kuwa shule hiyo kongwe na ambayo imekuwa ikitoa wataalamu mbali mbali imekuwa ina uhitaji wa kukarabatiwa na hivyo ili kuondokana na hali hiyo serikali inapaswa kutenga fedha kila mwaka ili kuweza kuirejesha shule hiyo katika mazingira mazuri yatakayowavutia wanafunzi.

Alileleza kuwa shule hiyo inakabiliwa na changamoto ya uchakavu mkubwa wa madarasa na nyumba za watumishi hali ambayo inasababisha mara nyingi wanafunzi kukosa mahala pazuri pa kujifunzia hivyo kuwakatisha tama kimasomo.

"tunaiomba na kuishauri serikali yetu sikivu iendelee kutenga fedha za
ukarabati kila mwaka kwa shule hizi kongwe ili kuzirudisha katika mazingira yake mazuri ikizingatiwa hii ni shule ya wanafunzi wenye vipaji maalum kiakili hali hii itawafnya wanafunzi wajitume zaidi katika masomo kwa kuwa na mazingi mazuri ya kujifunzia"aliongeza Shulla.

Aidha Shulla alitaja changamoto zingine zinazoikabili shule hiyo kongwe
kuwa ni pamoja na upungufu mkubwa wa walimu wa masomo ya sayansi ambapo hali hiyo inatokana na idadi kubwa ya wanafunzi wanaosoma masomo ya sayansi ikilinganishwa na idadi ya walimu.

Alifafanua kuwa tatizo hilo husababisha shule hiyo kutafuta walimu wa muda wa masomo ya Fizikia,kemia ,na hisabati ambao malipo yao ni makubwa sana kwa mwezi ambapo shule haina uwezo wa kumudu gharama hizo kila mwezi.

Aliwataka wahitimu hao kutumia elimu waliyoipata katika kutatua matatizo
yao na matatizo ya jamii yote kwa kufuata sheria na taratibu za nchi huku
wakijiepusha na uzembe ,ulevi,uvutaji bangi na matumiz ya madawa ya kulevya kwani hivyo vyote havina tija katika maendeleo.