Friday, November 28, 2014

Tuinue muziki wa injili kukuza maadili katika jamii: UDA



 Afisa Mtendaji Mkuu wa Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA), Bw John Samangu (kushoto) akikata utepe kuzindua rasmi albamu ya kwanza kutolewa na ya kwaya ya Kanisa la Kigango cha Mtakatifu Rita wa Kashia ijulikanayo kama 'Msifuni Bwana' jijini Dar es Salaam hivi karibuni. Wanaoshuhudia ni mwenyekiti wa Kigango cha Mt. Rita Bw. Frederick Msumali(kushoto) na waumini wengine.
 Afisa Mtendaji Mkuu wa Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA), Bw. John Samangu, akionyesha moja ya DVD wakati wa uzinduzi wa albamu ya kwaya ya Kigango cha kanisa la Mtakatifu Rita wa Kashia iitwayo 'Msifuni Bwana' jijini Dar es Salaam hivi karibuni. Wanaoshuhudia ni Padre Xavery Kassase, Paroko Msaidizi wa Parokia ya Kanisa Katoliki la Mavurunza (kulia) na Mwenyekiti wa Kigango cha Mt. Rita Bw. Frederick Msumali(kushoto).

Afisa Mtendaji Mkuu wa Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA), Bw John Samangu (kulia), akifungua moja ya kanda za albamu ya 'Msifuni Bwana' ya kwaya ya Kanisa la Kigango cha Mtakatifu Rita wa Kashia jijini Dar es Salaam hivi karibuni. Anayeshuhudia ni mwenyekiti wa Kigango cha Mt. Rita Bw. Frederick Msumali (kushoto). 

JAMII imeombwa kusaidia kuinua muziki wa injili unaofanywa na madhehebu mbalimbali ya dini ya nchini ili kusaidia kukuza maadili mema miongoni mwa wanajamii.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa albamu ya kwanza kuwahi kutambulishwa na kwaya ya kigango cha kanisa la Mtakatifu Rita wa Kashia jijini Dar es Salaam hivi karibuni, Afisa Mtendaji Mkuu wa Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA), Bw. John Samangu, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika uzinduzi huo, alisema kuwa albamu hiyo inayobeba jina la 'Msifuni Bwana' itasaidia kukuza maadili mema katika jamii, kwani nyimbo nyingi katika albamu hiyo zimebeba ujumbe mzuri.

Bw. Samangu alikuwa mtu wa kwanza kununua nakala tatu za DVD na albamu hiyo ambayo ni ya kwanza kuwahi kutambulishwa na kwaya ya kigango cha kanisa la Mtakatifu Rita wa Cascia tangu kuanzishwa kwake mwaka 2010.
  
Alisema kutokana na hali iliyopo sasa ya kuporomoka kwa maadili katika jamii, kuna umuhimu mkubwa wa taasisi kama makanisa kuhimiza watu kubadili tabia zao ili ziwe nzuri na zenye kupendeza. Alisema muziki wa injili ni miongoni mwa njia za kufikisha ujumbe utakaokuwa na athari chanya kwa walengwa wengi zaidi.

"Naisihi kwaya ya kigango cha kanisa la Mtakatifu Rita wa Kashia kuendelea kusambaza neno la Mungu, kwani kwa kupitia muziki pekee, idadi kubwa ya watu inaweza kufikiwa. Hii itasaidia jamii kubadilika na kuwa katika mlengo ulio sahihi," alisema Bw. Samangu.

Kwa upande wake, Paroko Msaidizi wa Parokia ya kanisa la Mavurunza, Padri Xavery Kassase, alisifu kitendo cha kwaya hiyo kutafsiri nyimbo zote katika albamu hiyo kwa kutumia lugha mbalimbali. Alisema kitendo icho kitasaidia albamu hiyo kuwafikia wasikilizaji wengi zaidi hata nje ya mipaka ya Tanzania.

"Kwa kuzitafsiri nyimbo kwenye lugha mbalimbali, inamaanisha kuwa mtaweza kusambaza albamu yenu nje ya nchi na hata kutumia mitandao ya kijamii kama YouTube ili watu wengi zaidi waweze kusikiliza na kuelewa ujumbe mzuri unaopatikana katika nyimbo hizi.  

Naiomba kwaya isiridhike na mafanikio waliyoyapata hadi kufikia sasa badala yake waendelee kufanya kazi kwa bidii kuhakikisha kuwa inakuwa miongoni mwa kwaya bora zaidi nchini Tanzania," alisema Padri Kassase.

Mbali na hilo, Padri Kassase aliwaomba watu wauunge mkono muziki wa injili kwani unabeba ujumbe wenye mafundisho yanayohimiza maadili mema katika jamii badala ya kushabikia nyimbo zinazoshabikia mambo maovu.