Waziri wa Maliasili Prof. Jumanne Maghembe (kushoto) akisalimiana na Waziri wa Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo kutoka Serikali ya Shirikisho la Ujerumani Dkt. Gerd Muller alipowasili katika uwanja mdogo wa ndege wa Matambwe uliopo ndani ya Hifadhi ya akiba ya Selous Mkoani Morogoro kwa ajili ya hafla ya makabidhiano ya ndege maalum aina ya Husky A-1C kutoka Serikali ya Ujerumani itakayosaidia kufanya doria za kupambana na ujangili katika hifadhi hiyo.
Sehemu ya kundi la Swala katika hifadhi ya akiba ya Selous.
Moja ya Twiga akiwa anakimbia katika hifadhi ya akiba ya Selous.
Sehemu ya wajumbe wa msafara wa Waziri Maghembe na Waziri wa Muller wakibadilishana mawazo katika hifadhi ya akiba ya Selous.
..............................................................
Serikali ya Ujerumani imetoa msaada wa ndege maalum aina ya "Husky A-1C Aircraft" kwa Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Malisili na Utalii kwa ajili ya kusaidia katika doria za kupambana na Ujangili katika Hifadhi ya Akiba ya Selous.
Msaada huo wenye thamani ya Euro 200,000 sawa na Tsh. 498,292,000, umekabidhiwa kwa Mhe. Waziri wa Maliasili Prof. Jumanne Maghembe na Waziri wa Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo wa Serikali ya Shirikisho la Ujerumani Dkt. Gerd Muller katika hafla fupi iliyofanyika Matambwe ndani ya pori la Akiba la Selous.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na Maafisa wa Ubalozi wa Ujerumani hapa nchini wakiongozwa na Balozi Mhe. Egon Konchanke, viongozi mbalimbali kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Mamlaka ya Wanyamapori Tanzania (TAWA), Mashirika ya Maendeleo ya Kimataifa ya FZS, WWF, GIZ na KFW.
Akizungumza katika hafla hiyo Waziri Maghembe amesema ndege hiyo itasaidia jitihada za Serikali za kupambana na Ujangili kwa kufanya doria katika anga ya hifadhi ya Akiba ya Selous na kusaidia kutoa taarifa za kiuhalifu pale itakapobainika na kuchukuliwa hatua stahiki za kukabiliana na uhalifu huo.
"Ndege hii tunayoshuhudia mapokezi yake leo ni ukombozi kwa Wanyamapori katika Pori hili la Akiba la Selous kwani itasaidia na kuimarisha doria za kupambana na ujangili ndani na kuzunguka eneo zima la hifadhi". Alisema Prof. Maghembe.
Waziri Maghembe ameishukuru Serikali ya Ujerumani kupitia kwa Waziri Muller kwa msaada huo na mingine ambayo wamekuwa wakiitoa kusaidia uhifadhi wa Wanamapori hapa nchini, Amebainisha kuwa misaada hiyo imekuwa na tija kubwa katika kuendeleza uhifadhi wa Wanyamapori ikilinganishwa na kipindi cha nyuma kabla ya kuwepo kwa misaada hiyo.
Waziri Maghembe alieleza kuwa sera ya Wanyamapori Tanzania inatambua ushirikiano wa wahisani na watu binafsi katika kuisaidia Serikali Kifedha na Kitaaluma kwenye eneo la uhifadhi, hivyo amewaomba wadau mbalimbali kuendelea kuipa ushirikiano Serikali katika jitihada zake za kuendeleza Uhifadhi wa Wanyamapori nchini.
Kwa upande wake Waziri wa Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo wa Ujerumani Dkt. Gerd Muller alimueleza Prof. Maghembe kuwa Serikali yake itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kuendeleza uhifadhi hapa nchini. Waziri huyo pia aliwapongeza Askari wa Wanyamapori kwa kazi nzuri wanayofanya ya kulinda Wanyamapori katika mazingira magumu ya porini.
Akizungumza kwa lugha ya Kijerumani huku ikitafsiriwa kwa Kiingereza na Mkalimani wake Dkt. Muller alisema ipo haja kubwa ya kuendelea kuwalinda Wanyamapori kwa nguvu zote kwa kuwa hawana hatia na kwamba walikuwepo katika mazingira yao ya asili kabla hata ya binadamu kuwepo hapo.
"Hawa viumbe hai wanaowindwa walikuwepo katika mazingira haya kabla ya sisi binadamu kuja hapa, Sote tunahitaji kuwalinda na kuishi kwa amani na viumbe hawa ndio kutakuwa na amani duniani kote" Alieleza Dkt. Muller.
Mapema akizungumza kabla ya tukio la kukabidhiwa ndege, Meneja wa Pori hilo la Akiba la Selous Bw. Mabula Misungwi alieleza baadhi ya changamoto kuu zinazoikabili hifadhi hiyo kuwa ni ujangili, miundombinu mibovu ya barabara kwa ajili ya doria na vifaa ikiwemo magari ya doria.
Msafara wa Waziri Maghembe na ugeni wake kutoka Serikali ya Shirikisho la Ujerumani walipata fursa ya kutembelea maeneo mbalimbali ya hifadhi ya Selous ikiwemo Matambwe na Behobeho ambayo inajulikana kama Serengeti ndogo na kujionea Wanyamapori mbalimbali wakiwemo Tembo, Twiga, Pundamilia, Swala, Nyani, Ngiri, Nyumbu na mandhari mazuri ya mto behobeho.
Hifadhi ya Akiba ya Selous ni moja ya hifadhi kubwa duniani ikiwa na ukubwa wa zaidi ya Kilomita za mraba 50,000. Hifadhi hii ipo ndani ya Mikoa mitano ya Tanzania ambayo ni Pwani, Morogoro, Lindi, Mtwara na Songea. Hifadhi hii imeathiriwa kwa kiasi kikubwa na ujangili kwani katika Sensa ya mwaka 2013 ilionesha idadi ya tembo katika hifadhi hiyo kuwa 13,000 idadi ambayo ni ndogo sana ikilinganishwa na ile ya mwaka 2003 ambayo ilikuwa 70,000.
(Picha na Hamza Temba - Wizara ya Maliasili na Utali #WWW.WIZARAyaMALIASILInaUTALII.BLOGSPOT.COM)