WAZIRI
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mnyaa Mbarawa,
ameipongeza Kampuni ya simu TTCL kwa juhudi inazofanya katika kutoa
huduma za Mawasiliano nchini na kuitaka kutumia kikamilifu fursa
ilizonazo ili kujiendesha kibiashara na kutoa gawio kwa Serikali.
Waziri
Mbarawa ameyasema hayo Mkoani Morogoro Jumatatu hii alipokuwa katika
ziara yake ya kukagua kazi zinazofanywa na Taasisi zilizo chini ya
Wizara yake na kutoa maelekezo mbalimbali ya kuboresha utendaji wa
taasisi hizo. Ziara ya Profesa Mbarawa katika Kampuni ya simu TTCL
ilimwezesha kupata taarifa fupi ya utendaji wa Kampuni ya TTCL Mkoa wa
Morogoro kwa mwaka 2015 pamoja na mipango na malengo ya Mkoa huo kwa
mwaka 2016 ikiwa ni pamoja na mikakati itakayowezesha kuyafikia malengo
hayo.
Aidha
Waziri Mbarawa alipata taarifa kuhusu utendaji wa Mkongo wa Taifa wa
mawasiliano na changamoto zinazokwamisha Mkongo huo kufanya kazi kwa
ufanisi. Uongozi wa TTCL Mkoa wa Morogoro ulimjulisha Waziri Profesa
Mbarawa kuwa, kikwazo kikubwa kinachokwamisha utendaji wa Mkongo wa
Taifa wa Mawasiliano uharibifu wa kukatwa kwa mtandao wa Mkongo huo
kunakofanywa na baadhi ya wakandarasi wa barabara na wakandarasi
wanaojenga mkongo wa kampuni ya simu ya Haloteli pamoja maporomoko ya
ardhi huko Njombe na Igavisenga.
Akijibu
hoja hizo, Profesa Mbarawa aliahidi kushirikiana na Menejimenti na bodi
ya TTCL katika kuzifanyia kazi changamoto hizo na kuwataka Wafanyakazi
wote kubadilika, kufanya kazi kwa juhudi kubwa na moyo wa uzalendo ili
kuiwezesha TTCL kuwa namba moja katika kutoa huduma za Mawasiliano
nchini na kumudu ushindani ulipo katika sekta hiyo hivi sasa. Aidha,
Waziri Mbarawa aliiagiza Menejimenti ya TTCL kuongeza kasi ya kupanua
huduma zote zinazotolewa na kampuni hiyo na hasa Mkongo wa Taifa wa
Mawasiliano ili kukidhi mahitaji makubwa ya huduma hiyo na fursa kubwa
ya kibiashara iliyopo kutoka kwa makampuni yanayotoa huduma za tehema.
Baadhi
ya Wafanyakazi wa TTCL walimuuliza Waziri Mbarawa kuhusu tetesi
zilizopo kuwa anakusudia kuanzisha taasisi nyingine na kuikabidhi jukumu
la kusimamia Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano ambao tangu kuanzishwa
kwake, umekuwa chini ya usimamizi wa TTCL ambapo Waziri Mbarawa
alikanusha tetesi hizo na kusema kuwa, Serikali ilishafanya uamuzi kwa
kuikabidhi TTCL jukumu la kuusimamia na kuuendesha Mkongo wa Taifa wa
Mawasiano na hivyo hakuna mpango mwingine tofauti na uamuzi huo.
Waziri
Mbarawa aliongeza kuwa kuwa, Serikali itaiongezea TTCL jukumu jingine
la kusimamia kituo cha kutunzia kumbukumbu (Data Center) kinachotarajia
kuanza kazi muda mfupi ujao pamoja na na kuahidi kusaidia kuiwezsha TTCL
kupata masafa ili kuongeza uwezo wake wa kutoa huduma.