Saturday, April 04, 2015

TANZANIA KUWA KITUO CHA USULUHISHI




TANZANIA KUWA KITUO CHA USULUHISHI

Tanzania inatarajia kuzindua kituo cha kimataifa cha usuluhishi wa migogoro ya kibiashara kutokana na kukua kwa sekta ya uwekezaji ikiwamo mafuta na gesi nchini.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Godfrey Simbeye alisema kituo hicho kitazinduliwa Juni mwaka huu na kitasimamia na kutatua migogoro yote ya kibiashara itakayojitokeza katika kipindi hiki cha ugunduzi wa gesi na mafuta.
Simbeye alisema, kuanzishwa kwa kituo hicho kunatokana na kuongezeka kwa wawekezaji nchini, kuboresha biashara na kuongezeka kwa wafanyabiashara wakubwa hasa baada ya kuzinduliwa kwa sekta ya mafuta na gesi.
"Rwanda tayari imeanzisha kituo kama hicho, kimesaidia kutatua migogoro ya kibiashara dhidi ya wawekezaji na wafanyabiashara," alisema.
Alisema hayo juzi, wakati akielezea maandalizi ya mkutano wa kimataiafa wa usuhuhishi wa migogoro ya kibiashara utakaofanyika jijini Dar es Salaam,  Aprili 9 - 10 mwaka huu.
Simbeye alisema lengo la mkutano huo ni kujadili namna ya kutatua migogoro ya kibiashara na kijamii nje ya mahakama bila kufikishwa kwa kesi hizo mahakamani.
"Mkutano huu utashirikisha nchi za Afrika Mashariki. Migogoro  hiyo itatatuliwa bila kesi kufikishwa mahakamani kwa sababu tunaona mashauri mengi yanatumia muda mrefu kutolewa hukumu lakini tukishiriana na Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS) na TPSF tunaweza kutatua migogoro hiyo nje ya mahakama," alisema Simbeye.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), Kaleb Gamaya alisema kupitia mkutano huo, washiriki watapata nafasi ya kuangalia  jinsi ya kutatua migogoro nje ya utaratibu wa mahakama kama nchi zilizoendelea zinavyofanya.
"Usuluhishi wa migogoro unaofanyika mahakamani unaweza kumalizika baada ya miaka mitatu, hivyo kibiashara unakuwa umeathiri uchumi kwa sababu ya muda wa kupitia mashauri, ndiyo maana tukaona kuna haja ya kujitosa kuanzisha utaratibu huu," alisema Gamaya.
Aliongeza: "Lengo la TLS ni kujadili na kushawishi wanachama wetu kuwapo katika  mkutano huu na washiriki watapata elimu na faida ya usuluhishi nje ya mahakama," alisema.
Alisema mkutano huo wa tatu kufanyika Afrika, utajadili migogoro ya mafuta na gesi kwa sababu ni kitu kipya nchini na kwamba mikutano kama hiyo ilishawahi kufanyika Nairobi na Addis Ababa miaka mitatu iliyopita.
Mratibu wa mkutano huo kutoka Mtandao wa kibiashara wa Afrika Mashariki, Martha Yeronimo alisema watu zaidi ya 200 wanatarajia kushiriki kutoka ndani na nje ya Tanzania.